Thursday, March 28, 2013

TAMASHA LA WAANDISHI WA HABARI LAHAMIA TCC CLUB



Na Prince Asia

BONANZA la vyombo mbalimbali vya habari lililopangwa kufanyika Aprili 6 mwaka huu viwanja vya Leaders Klabu likiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), sasa litafanyika viwanja vya Sigara (TCC), Chang’ombe pia Dar es Salaam. Katibu wa TASWA, Amir Mhando amesema uamuzi wa kuhamishia bonanza hilo TCC umechukuliwa na sekretarieti ya TASWA kutokana na maombi ya waandishi wengi wa michezo kwa vile siku hiyo kuna mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika kati ya timu ya soka ya Azam na Barrack Young Controllers ya Liberia  itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Amesema Azam ni timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye michuano ya Afrika kwa ngazi ya klabu baada ya Simba na Jamhuri ya Pemba kutolewa katika raundi ya awali.
“Tunaamini kwa bonanza kufanyika Sigara itakuwa rahisi kwa wadau wetu kushiriki kwenye bonanza na wale wengine watakaohitaji kwenda uwanjani wafanye hivyo wakitokea Sigara kwa hakuna umbali mrefu na kisha warejee kujumuika na wenzao mpaka mwisho,”.
Mhando alisema TASWA inawaomba radhi wadau wake kwa mabadiliko hayo, lakini yakiwa na lengo la kujenga na kuwa pamoja na Azam kuhakikisha wanashirikiana nao kwa namna mbalimbali siku hiyo.
Bonanza hilo limedhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
Bonanza hilo ambalo litahusisha wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote vitakavyoshiriki na pia kutakuwa na burudani ya muziki kutoka katika moja ya bendi kubwa za muziki wa dansi hapa nchini, ambayo itatangazwa siku zijazo.

Chanzo Bin Zubery