KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, amesema suala la gesi asili linaleta mvutano kwa sababu
ya maslahi ya watu wachache.
Watu wanaoendekeza mgogoro katika sakata hilo ni wale waliofilisika
kifikra, hawajui Katiba na hawajui kuwa wananchi ndio walinzi wa kwanza
wa rasilimali zao.
Alisema kuwa wanaokuja na hoja ya kusema ni siasa, wanakurupuka kwani
wao kama wanasiasa ni lazima kupiga kelele kupinga dhuluma inayotaka
kufanywa na serikali dhidi ya wananchi hao.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Dk. Slaa, alisema Katiba ya nchi
pamoja na udhaifu iliyonao, imeainisha vema misingi ya kusimamia
rasilimali za taifa kwa usawa bila ubaguzi wala dhuluma.
Alisema kuwa katika suala hilo hawatafuti umaarufu wowote wa kisiasa,
na hivyo kuhoji ni nani anaweza kutafuta umaarufu katika shida za watu?
Dk. Slaa aliongeza kuwa Mtwara ni sehemu tu ya Tanzania, hivyo
wananchi wa huko na Lindi wana haki ya kunufaika na rasilimali
iliyopatikana kwao.
“Serikali inasisitiza kujenga mitambo Kinyerezi kwa kuwa wanataka
kuleta gesi hiyo Dar es Salaam ili kunufaika wao kwanza, jambo ambalo ni
la kiubaguzi,” alisema.
Kwa mujibu wa katibu huyo, serikali ingekuwa wazi kwa kuwaambia
wananchi inalinda Katiba ipi; maana iliyopo inawapa wananchi haki ya
kulinda rasilimali zao na kunufaika nazo.
Alifafanua kuwa mkazo unaopaswa kuwepo kwa maendeleo ya taifa,
unazungumzia kuondoa maadui watatu yaani ujinga, maradhi na umaskini.
“Wananchi wa Mtwara ni maskini, mkoa wao umetelekezwa muda mrefu,
wamekopwa korosho yao, sasa wamepata gesi na wanayo haki ya kudai
wanufaike nayo ili nao wapate viwanda, shule na hospitali nzuri,”
alisema.
Dk. Slaa alisema mikoa hiyo haijawahi kuwa na hospitali ya rufaa,
hivyo wanaionya serikali isiendeshe shughuli za uchumi kwa maslahi ya
watu wachache.
Alisisitiza kuwa hakuna sababu za kutokuwekeza mitambo ya gesi Mtwara
na Lindi ili isaidie ukuaji wa maeneo hayo kiuchumi na kwamba jambo hilo
wala halina siasa.
Alisema ni jukumu la kila mwananchi kulinda utajiri wa taifa lake
kwani wao ndio wamiliki, hivyo hawapaswi kutegemea hisani ya serikali na
badala yake serikali inapaswa kuwajibuka kwao.
Kauli hiyo ya Dk. Slaa inakuja siku chache baada ya Waziri wa Nishati
na Madini kuwabeza wananchi wa Mtwara walioandamana wakiongozana na
baadhi ya wanasiasa kupinga usafirishwaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda
Dar es Salaam.
Desemba 27, wananchi wa Mtwara waliandamana kupinga hatua ya serikali
kutaka wasafirishe gesi hadi Dar es Salam na kuwaacha wao wakiwa hawana
kitu.
Januari 2, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo,
akizungumza na waandishi wa habari alipinga hatua hiyo ya wananchi na
kusema jambo hilo limevamiwa na wanasiasa.
“Hiyo gesi inayowafanya wanasiasa wawashawishi wakazi wa Mtwara
kuandamana haiko Mtwara wala Lindi, bali iko katika mipaka ya Tanzania
ndani ya kina kirefu cha bahari na kwa hilo kila Mtanzania ana haki ya
kutumia,” alisema.
Waziri Muhongo alisema ni jambo la kusikitisha kuona wakazi wa Mtwara
wakiandamana kwa ajili ya gesi wakati walipa kodi wa Tanzania
hawajaandamana kwa ajili ya rasilimali zinazotoka maeneo mengine kwenda
kutumika Mtwara.
Alikwenda mbali na kulaumu kile alichokiita wanasiasa kujiingiza katika sakata hilo na kuwahimiza wananchi waandamane.
|
No comments:
Post a Comment