Lowassa: CCM hodari wa kuiba kura
Dar es Salaam. Mgombea wa urais
kupitia Chadema, Edward Lowassa ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba
kura hivyo akawataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili hata
sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo.
Lowassa
ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa Ukawa
uliojitokeza jana kumpokea katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo
Buguruni kuwa ili kufanikisha ushindi wa kuwawezesha kuingia ikulu
hawana budi kushikamana, kushawishiana kupiga kura kwa wingi na
kuzilinda Oktoba 25.
Kauli hiyo ya Lowassa ambaye
amelelewa kisiasa na CCM tangu alipojiunga akiwa mdogo mwaka 1977,
inaendeleza tuhuma ambazo hutolewa na vyama vya upinzani kuwa chama
hicho huchakachua matokeo wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.
“Tukiwa
na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi sana.
Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate
angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa
katika hotuba yake iliyokuwa inakatishwa na kushangiliwa na na salamu
ya CUF ya “Hakiii” na kujibiwa “kwa wote.”
“Hodari sana
wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura nyingi za kutosha hata wakiiba kura
hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema ‘piga kura, linda kura’ na
sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.”
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kwa simu kuhusu madai
hayo, alijibu kwa ujumbe wa maneno kuwa asingeweza kuzungumza bali
atumiwe ujumbe, na alipotumiwa ujumbe huo hakujibu.
Lubuva: Aeleze wanaibaje
Akizungumzia
madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji
mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura.
“Ili
kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya tuhuma
hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo nitaeleza kitu
ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu aliyekuwa
serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.”
Tume
huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo kuna
mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi yake
ifanye utafiti wa kina.
“Naomba nieleweshwe kura huwa
zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura
zetu wakati upande mwingine unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio
vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva.
Lowassa ambaye
alihamia Chadema siku 11 zilizopita na baadaye kuteuliwa kugombea urais
kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema safari ya Ikulu
itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo Watanzania
watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza undani
kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura.
Kiongozi
huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka wanawake nao kujitokeza kwa
wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa wameshapika vyakula majumbani
mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda kura.
Lowassa
alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia ya nchi kukuza uchumi na
kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.”
Ukawa kutoyumba
Mbunge
huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema Ukawa ipo imara
haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu kujipitisha
kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke.
“Wanakuja
kupitisha hela na kuhongahonga lakini viongozi wapo imara…hawahongeki
hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya ufukuzi ufukuzi, nawaambia
muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika.
Alisema
kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa Ukawa ikiingia madarakani
nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha wafanyabiashara kukimbiza fedha
zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli.
“Waongo
wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali, Ukawa ikiingia madarakani
nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela zenu..tupo imara,”
alisema.
Juma Duni afafanua
Mgombea
mwenza wa urais wa Ukawa, Juma Duni Haji alisema hajahamia Chadema
kutafuta vyeo kwa kuwa ameondoka akiwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na
waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na hatua yake hiyo ni
kutimiza za kuing’oa CCM madarakani.
“Ni vizuri
mkaelewa kwamba tutafanya kosa kubwa tusipofika ikulu mwaka huu,
tutahitaji kusubiri miaka 50 zaidi maana jamaa hawa wakija kutulia balaa
yao ni mara 100 ya wanayoyafanya. Wanaoleta mabadiliko ni vijana siyo
wazee,” alisema Duni Haji.
Alisema Ukawa wanatakiwa
kushirikiana kwa dhati na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa mwaka huu ni wa
mageuzi na kila mmoja ana wajibu wa kufanya kampeni ya kuiondoa CCM ili
kutafuta hatima bora ya nchi.
Kauli ya Mbowe
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuna nguvu nyingi zinatumika kuivunja
Ukawa lakini umoja huo utabaki kuwa imara na kutimiza malengo yake ya
kushika dola mwaka huu kwa nguvu za Mungu.
Alisema
vyama vya upinzani vimefanya siasa zao kwa shida kwa miaka 25 huku
baadhi ya makada wakifungwa, kufukuzwa kazi, ndoa kuparaganyika,
kufungwa au kufunguliwa kesi mahakamani lakini miezi minane iliyopita
imekuwa migumu zaidi kutokana na baadhi ya watawala kupatwa na hofu
baada ya Ukawa kujiimarisha.
“Safari yetu imebaki
kidogo tufike tunakoelekea. Sasa akitokea kiongozi mmoja wetu bila
kujali ni wa chama gani akaona kwamba malengo yetu siyo ya muhimu kuliko
fursa binafsi, huyo hatufai,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Alisema
maandamano ya leo kumsindika Lowassa kuchukua fomu yataanzia CUF na
kupitia ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi Ilala hadi NEC kabla ya
kurudi ofisi za Chadema Kinondoni.
Mwenyekiti wa NLD,
Dk Emmanuel Makaidi aliwataka wafuasi wa Ukawa kujitokeza kwa wingi
kumsindikiza mgombea wa urais kupitia umoja huo na ikiwezekana kila
mfuasi apeleke watu 10.
Mbatia amvaa JK
Mwenyekiti
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Ukawa itaendelea kuhubiri amani
siku zote ili CCM na vyombo vya dola visipate sababu ya kuwatuhumu na
kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.
Alisema Rais
Jakaya Kikwete alihubiri chuki dhidi ya wapinzani kwa kuwaita maadui
siku alipozungumza na wafuasi wa CCM baada ya kumpokea mgombea wa urais
kupitia chama hicho, Dk John Magufuli alipotoka kuchukua fomu za
kuwania.
“Sikuamini kama Rais Kikwete angesema maneno
yale eti anawaambia wana-CCM wana mikakati ya kila aina ya kushinda na
kwamba ‘msiogope kujihadhari na nguvu za adui’. Yaani sisi wapinzani ni
adui? Ukianza kuwaita wenzio adui wakati wewe ni amiri jeshi mkuu, nchi
hii unaipeleka wapi?” alihoji Mbatia.
Malim Seif apongeza
Katibu
Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwashukuru wafuasi wa Ukawa
waliojitokeza kumpokea Lowassa wakati wa ziara ya kutembelea ofisi zao
na kwamba moyo huo uendelee hadi Oktoba 25 siku ya kupiga kura.
“Hakuna
silaha kubwa kuliko umoja, ushirikiano na mshikimano. Tukishirikiana
tukawa wa kweli wa nafsi zetu bila shaka Lowassa anasubiri kuapishwa tu
na sisi Zanzibar tumeshamaliza kazi,” alisema Maalim Seif na
kushangiliwa na umati wa wafuasi hao.
Hali ilivyokuwa
Mapema
kabla ya Lowassa hajawasili Buguruni wafuasi wa CUF walianza
kujikusanya taratibu saa 4 asubuhi kwa kuzunguka na ngoma barabara za
Uhuru na za mitaa kuingia ofisi za chama hicho.
Baadaye
umati huo uliongezeka kiasi cha kufunga barabara ya Uhuru kwa muda
wakati Lowassa anaingia saa 6:20 mchana na kupokelewa na Maalim Seif,
Makaidi, Mbatia na viongozi waandamizi wa Ukawa.
Idadi hiyo ya watu iliwapa kibarua maofisa usalama wa Ukawa walioonekana wakihaha kutengeneza njia ili viongozi hao wapite.
Baada
ya viongozi hao kuwahutubia wafuasi hao, waliingia katika ukumbi wa
Mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi saa 7:15 mchana na kufanya mazungumza
ya takriban saa moja na baadaye viongozi kutoka nje ya CUF kuondoka.
Nafasi ya Lipumba
Kikao
cha Baraza Kuu kilijadili nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa na Profesa
Lipumba na suala hilo liliachiwa Mkutano Mkuu wa chama ambao utaitishwa
baada ya miezi sita kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kufanya uchaguzi huo
kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akitoa taarifa ya kikao
hicho, Maalim Seif alisema Baraza Kuu limeunda kamati maalum ya watu
watatu itakayofanya kazi na katibu mkuu kwa miezi sita kabla ya Mkutano
Mkuu kukaa na kumchagua mwenyekiti na makamu wake, nafasi ambazo ziko
wazi.
Waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Twaha
Taslima ambaye ni mwenyekiti na wajumbe wawili ambao ni Aboubakary
Khamis Bakary (Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar) na Sererina Mwijage
(mbunge mstaafu wa viti maalumu.