REGINALD MENGI AHOFIA KUULIWA NA SERIKALI YA KIKWETE,SOMA HAPA KUJUA::
Mwenyekiti wa Makampuni
ya IPP, Dk. Reginald Mengi amesema anahofia usalama wa maisha yake,
kufuatia habari iliyoandikwa katika gazeti moja la kila wiki kwamba,
Rais Jakaya Kikwete aliapa kupambana naye jambo ambalo limempa hofu
kubwa.
Kadhalika,
amelalamikia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari Maelezo
kwa kukaa kimya na kuacha kutoa ufafanuzi dhidi ya tuhuma hizo, huku taarifa
hizo zikiendelea kusambazwa.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mengi alisema kuwa tuhuma
zilizotolewa dhidi yake kuwa yeye ni kinara wa kuhujumu serikali ya Rais
Kikwete siyo za kweli.
Dk.Mengi alisema
amesoma kwa masikitiko makubwa habari iliyochapishwa Machi 23, mwaka huu na
gazeti la Taifa Imara, yenye kichwa cha habari 'Zitto amchongea Mengi kwa JK'
ambapo pamoja na mambo mengine inasema kuwa Zitto Kabwe amemchongea Dk. Mengi
kwa Rais Kikwete kwamba ndiye kinara wa kuhujumu serikali yake.
Alisema habari
hiyo ambayo chanzo chake kimeelezwa kwamba ni Ikulu, iliendelea kueleza kuwa
Zitto alikutana na Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuwasilisha bungeni ripoti
ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na kashfa ya Escrow
ambayo Zitto alikuwa ni mwenyekiti wake.
"Habari hiyo
inasema kwamba katika mazungumzo yake na Rais Kikwete Zitto amenukuliwa
akimueleza mkuu huyo wa nchi kuwa anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara
ni Mengi," alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema
habari hiyo ambayo nakala yake ameiambatanisha kwenye taarifa yake, inasema
yeye Zitto , binafsi amekuwa akishawishiwa na Dk. Mengi kuiangusha serikali ya
Rais Kikwete.
Hata hivyo, Dk. Mengi
alisema katika habari hiyo Zitto alikwenda mbali zaidi kumueleza Rais Kikwete
kuwa Dk. Mengi ameapa kuwa Rais Kikwete akimaliza muda wake wa Urais
atamshughulikia kwa nguvu zake zote.
Alisema habari hiyo
imeeleza kwamba baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliapa kupambana na Dk.
Mengi na akamshukuru Zitto kwa kumpa taarifa hizo.
Mengi alisema tuhuma
zilizotolewa kuhusu nia yake ya kutaka kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na
kumshughulikia baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, zimemshtua sana na tamko
la kwamba Rais Kikwete aliapa kuwa atapambana na yeye zimempa hofu kuhusu
mustakabali wa maisha yake.
Alisema kuwa hofu
yake kubwa inasababishwa na Ikulu na Idara ya habari Maelezo kukaa kimya kwa
zaidi ya wiki tatu bila kutoa ufafanuzi wowote.
"Najua umakini wa
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya habari Maelezo katika kutoa
ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu Rais, lakini katika hili
nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo
kusambaa,"alisema Dk. Mengi.
Aliongezea kusema
kuwa," hofu yangu inazidi kuwa kubwa kwa sababu Rais ni Mkuu wa Majeshi ya
ulinzi na usalama. Kauli yake kama ilivyonukuliwa na gazeti hili kwamba
atapambana na mimi inawezekana kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola
kuniangamiza," alisema.
Alitolea mfano
mwaka 1170, Askofu Mkuu wa Canterbury nchini Uingereza aliuawa baada ya walinzi
wa mfalme kusikia mfalme akisema "hakuna anayeweza kuniondolea huyo
mkorofi?". Walinzi wake wakadhani mfalme ameagiza wamuue Askofu huyo na
wakamuua, alisema.
CHANZO: NIPASHE