PADRI Evarist Mushi (55), aliyeuawa juzi kwa kupigwa risasi na watu
wasiojulikana Zanzibar, anatazamiwa kuzikwa Kitope katika eneo
lililotengwa la makaburi ya mapadri.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Askofu wa Kanisa Katoliki,
Jimbo la Zanzibar, Augostino Shao, alisema maandalizi ya maziko
yanaendelea vizuri.
“Tunatarajia kuupumzisha mwili wa marehemu Mushi katika makaburi ya
Kitope ambako kuna sehemu maalumu ya kuzikwa mapadri,” alisema.
Marehemu Mushi atakuwa Padri wa tatu kuzikwa eneo hilo mkoani Kaskazini
Unguja, ambako alisema kwa sasa ni mapema kujua viongozi
watakaohudhuria maziko.
Akielezea jinsi alivyopokea taarifa ya kifo cha Padri Mushi, ambaye
alikuwa Msaidizi wake Mkuu, Askofu Shao alisema alipokea wakati
akiendesha ibada ya kawaida ya Jumapili katika Kanisa la Minara Miwili.
“Nilikuwa naongoza ibada, lakini wenzangu tayari walikuwa wamepata taarifa ya kifo cha Padri Mushi.
Nilikuwa naye asubuhi saa 12 tukaagana, naye akaenda kuongoza misa Mtoni katika Kanisa la Beit-el-Ras,” alisema.
Askofu Shao alivitaka vyombo vya ulinzi, kufanya kazi za kusaka wahalifu kwani jamii tayari imeanza kupoteza imani.
Padri Mushi aliuawa kwa risasi tatu alizopigwa kichwani na watu
wasiojulikana juzi saa moja asubuhi, akienda kanisani kuongoza ibada.
Akiwa katika gari lake aina ya Toyota Hilux Surf, Padri Mushi alipigwa risasi kichwani kupitia dirisha la mlango wa kulia.
Mauaji hayo yalifanyika wakati akikata kona kuingia kanisani, ambako
watu hao walikuwa wakimsubiri wakiwa na usafiri wa Vespa na baada ya
kumpiga risasi walikimbia.
Kutokana na hali hiyo, gari la Padri Mushi lilipoteza mwelekeo na
kupamia ukuta wa nyumba iliyo meta chache kutoka Kanisa la Mtakatifu
Theresia, ambako alikuwa akienda.
No comments:
Post a Comment