Huyu ndiye Edward Lowassa ‘MwanaCCM Mtiifu’
Edward Ngoyai Lowassa, ni mmoja kati ya wanachama wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) nchini Tanzania. Jina lake linatajwa kuwa miongoni mwa watu wenye nafasi kubwa ya kuwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania.Mengi yanazungumzwa, mengi yanasemwa juu ya sifa na uwezo wake, makala haya hayalengi kujadili uwezo wake kama kiongozi ila nafasi yake kama mwanachama halali na mtii kwa Chama Cha Mapinduzi.
Februari 18, 2014, Edward Lowassa pamoja na makada wengine wa Chama Cha Mapinduzi walipewa adhabu ya miezi 12 kwa kukiuka kanuni za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i). Kifungo hicho kimemalizika siku chache zilizopita.
Maswali mengi waliyonayo watanzania ni je nini hasa hatma ya Lowassa? Na je kihistoria Lowassa ni nani hasa ndani ya chama cha mapinduzi?
Bahati mbaya sina majibu ya swali la kwanza, hata hivyo nina majibu ya swali la pili na hilo linaweza kutusaidia kujibu lile la kwanza. Je Lowassa ni mwanachama wa aina gani wa CCM?
Jibu rahisi ni Lowassa ni ‘Mwana CCM Mtiifu’. Hebu tuitazame kidogo historia yake ndani ya chama. Edward Ngoyai Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 na katika Kijiji Cha Ngarash huko Monduli, Lowassa ni mtoto mkubwa wa kiume kwa mzee Ngoyai Lowassa.
Kielimu, Lowassa ana Shahada ya Uzamivu (masters degree) katika Maendeleo kutoka Chuo Kikuu Cha Bath nchini Uingereza aliyohitimu mwaka 1984, na kabla ya hapo alihitimu shahada ya kwanza katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977.
Kikazi, Lowassa amekulia na kufanya kazi zaidi ndani ya CCM na serikali yake. Lowassa amejiunga na CCM akiwa chuo kikuu cha Dar es Salaam. Huko alikuwa mwanachama hai na baadae kiongozi wa Tanganyika African National Union (TANU) Youth League (baadae CCM Youth League). Mara baada ya kuhitimu masomo, aliajiriwa na CCM kama katibu msaidizi na baadaye katibu wa wilaya.
Hili pekee linatosha kuonyesha kuwa Lowassa amekulia katika misingi ya chama, ameanza kuaminiwa na chama akiwa kijana mdogo (bila shaka baada ya viongozi wa chama kujua weledi, uzalendo na utiifu wake) na ameshiriki toka ujana wake kwenye ujenzi wa CCM na Tanzania kwa ujumla. Akiwa kijana ndani ya CCM alipata kuwa msaidizi wa Mzee Rashid Mfaume Kawawa, Daudi Mwakawago na Horace Kolimba.
Mzee Kawawa alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na Tanzania, mmoja wa waasisi wa chama na taifa letu. Bila shaka Lowassa alijifunza mengi kutoka kwake, na kama sio utiifu wa hali ya juu na uzalendo wake kwa chama na taifa, asingekweza kufanya kazi na mzee Kawawa,anayesifika kuwa na misimamo ya hali ya juu.
Pia Lowassa ni Luteni wa jeshi, licha ya kupigana vita dhidi ya Idd Amin nchini Uganda mwaka 1978/1979, pia akiwa jeshini alifanya kazi kwa ukaribu na Rais Jakaya Kikwete pamoja na katibu mkuu wa CCM wa sasa Mh Abdulrahman Kinana ambao wote ni makada wa CCM kwa miaka mingi. Wote tunajua kuwa jeshini ndiko kulikobobea kwa kufunzwa uzalendo na utiifu wa hali ya juu.
Mwaka 1985,Lowassa aliteuliwa kuwa Mbunge kupitia Umoja Wa vijana CCM (UVCCM), sambamba na Mama Anne Makinda (Spika wa Bunge la sasa) na Jenerali Ulimwengu. Mwaka 1990 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Monduli akipeperusha bendera ya CCM ambako amekuwa mwakilishi hadi leo.
Toka mwaka 1977 Lowassa amekuwa akiaminiwa na CCM na hakuwahi kukiangusha, amekwisha kabidhiwa dhamana nyingi za uongozi zenye kumpa dhamana ya kusimamia na kutekeleza ilani za chama, nyadhifa ambazo kila wakati alizitekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu. Lowassa amekwisha kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania (2005-2008), Waziri wa Maji na Mifugo (2000-2005), Ardhi na Makazi (1993-1995), Haki na Mambo ya Bunge (1990-1993), na Mazingira na Mapambano dhidi ya umasikini katika ofisi ya Makamu wa Rais.
Utiifu wa Lowassa kwa chama ulijidhihirisha wazi mwaka 2008 alipokubali kwa ridhaa yake kuachia nafasi yake ya Uwaziri Mkuu ili kulinda heshima ya serikali nzima, Chama tawala CCM na pia ili kuepuka mgawanyiko miongoni mwa wanachama, wananchi na viongozi. Huu ni uungwana na uzalendo wa hali ya juu, wenye moja ya vielelezo vya utawala bora.
Mwaka 2014 tumeshuhudia sakata la Escrow ambapo pamoja na kuwa na ushahidi wa wazi wa pesa kwenye akaunti zao, baadhi ya Mawaziri waligoma kuwajibika kwa hiari yao na wengine kusimamishwa kazi na Rais. Lowassa alijiuzuru kwa tuhuma tu, ambazo hazikuwa na mashiko wala ushahidi yakinifu, wala walau kupewa nafasi kuhojiwa na kamati teule ya bunge.
Kwa maelezo hayo nachelea kusema kuwa, Lowassa amekuwa mwanachama mtiifu kwa Chama Cha Mapinduzi kwa miaka mingi na hajawahi kukiangusha chama wala serikali wala taifa kwa namna yoyote ile. Watu kama hawa wanastahili pongezi na ni mfano wa kuigwa ndani na nje ya chama.
No comments:
Post a Comment