Monday, August 10, 2015

Lowassa: CCM hodari wa kuiba kura

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na mgombea urais wa muungano wa Ukawa, Edward Lowassa wakiwapungia mkono wananchi waliofurika makao makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame 
By Nuzulack Dausen na Suzan Mwillo, Mwananchi
Dar es Salaam. Mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo akawataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo.
Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa Ukawa uliojitokeza jana kumpokea katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni kuwa ili kufanikisha ushindi wa kuwawezesha kuingia ikulu hawana budi kushikamana, kushawishiana kupiga kura kwa wingi na kuzilinda Oktoba 25.
Kauli hiyo ya Lowassa ambaye amelelewa kisiasa na CCM tangu alipojiunga akiwa mdogo mwaka 1977, inaendeleza tuhuma ambazo hutolewa na vyama vya upinzani kuwa chama hicho huchakachua matokeo wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.
“Tukiwa na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi sana. Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa katika hotuba yake iliyokuwa inakatishwa na kushangiliwa na na salamu ya CUF ya “Hakiii” na kujibiwa “kwa wote.”
“Hodari sana wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura nyingi za kutosha hata wakiiba kura hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema ‘piga kura, linda kura’ na sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kwa simu kuhusu madai hayo, alijibu kwa ujumbe wa maneno kuwa asingeweza kuzungumza bali atumiwe ujumbe, na alipotumiwa ujumbe huo hakujibu.
Lubuva: Aeleze wanaibaje
Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura.
“Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.”
Tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi yake ifanye utafiti wa kina.
“Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva.
Lowassa ambaye alihamia Chadema siku 11 zilizopita na baadaye kuteuliwa kugombea urais kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema safari ya Ikulu itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo Watanzania watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza undani kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura.
Kiongozi huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka wanawake nao kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa wameshapika vyakula majumbani mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda kura.
Lowassa alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia ya nchi kukuza uchumi na kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.”
Ukawa kutoyumba
Mbunge huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema Ukawa ipo imara haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu kujipitisha kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke.
“Wanakuja kupitisha hela na kuhongahonga lakini viongozi wapo imara…hawahongeki hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya ufukuzi ufukuzi, nawaambia muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika.
Alisema kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa Ukawa ikiingia madarakani nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha wafanyabiashara kukimbiza fedha zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli.
“Waongo wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali, Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela zenu..tupo imara,” alisema.
Juma Duni afafanua
Mgombea mwenza wa urais wa Ukawa, Juma Duni Haji alisema hajahamia Chadema kutafuta vyeo kwa kuwa ameondoka akiwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na hatua yake hiyo ni kutimiza za kuing’oa CCM madarakani.
“Ni vizuri mkaelewa kwamba tutafanya kosa kubwa tusipofika ikulu mwaka huu, tutahitaji kusubiri miaka 50 zaidi maana jamaa hawa wakija kutulia balaa yao ni mara 100 ya wanayoyafanya. Wanaoleta mabadiliko ni vijana siyo wazee,” alisema Duni Haji.
Alisema Ukawa wanatakiwa kushirikiana kwa dhati na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa mwaka huu ni wa mageuzi na kila mmoja ana wajibu wa kufanya kampeni ya kuiondoa CCM ili kutafuta hatima bora ya nchi.
Kauli ya Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuna nguvu nyingi zinatumika kuivunja Ukawa lakini umoja huo utabaki kuwa imara na kutimiza malengo yake ya kushika dola mwaka huu kwa nguvu za Mungu.
Alisema vyama vya upinzani vimefanya siasa zao kwa shida kwa miaka 25 huku baadhi ya makada wakifungwa, kufukuzwa kazi, ndoa kuparaganyika, kufungwa au kufunguliwa kesi mahakamani lakini miezi minane iliyopita imekuwa migumu zaidi kutokana na baadhi ya watawala kupatwa na hofu baada ya Ukawa kujiimarisha.
“Safari yetu imebaki kidogo tufike tunakoelekea. Sasa akitokea kiongozi mmoja wetu bila kujali ni wa chama gani akaona kwamba malengo yetu siyo ya muhimu kuliko fursa binafsi, huyo hatufai,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Alisema maandamano ya leo kumsindika Lowassa kuchukua fomu yataanzia CUF na kupitia ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi Ilala hadi NEC kabla ya kurudi ofisi za Chadema Kinondoni.
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi aliwataka wafuasi wa Ukawa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wa urais kupitia umoja huo na ikiwezekana kila mfuasi apeleke watu 10.
Mbatia amvaa JK
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Ukawa itaendelea kuhubiri amani siku zote ili CCM na vyombo vya dola visipate sababu ya kuwatuhumu na kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alihubiri chuki dhidi ya wapinzani kwa kuwaita maadui siku alipozungumza na wafuasi wa CCM baada ya kumpokea mgombea wa urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli alipotoka kuchukua fomu za kuwania.
 “Sikuamini kama Rais Kikwete angesema maneno yale eti anawaambia wana-CCM wana mikakati ya kila aina ya kushinda na kwamba ‘msiogope kujihadhari na nguvu za adui’. Yaani sisi wapinzani ni adui? Ukianza kuwaita wenzio adui wakati wewe ni amiri jeshi mkuu, nchi hii unaipeleka wapi?” alihoji Mbatia.
Malim Seif apongeza
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwashukuru wafuasi wa Ukawa waliojitokeza kumpokea Lowassa wakati wa ziara ya kutembelea ofisi zao na kwamba moyo huo uendelee hadi Oktoba 25 siku ya kupiga kura.
“Hakuna silaha kubwa kuliko umoja, ushirikiano na mshikimano. Tukishirikiana tukawa wa kweli wa nafsi zetu bila shaka Lowassa anasubiri kuapishwa tu na sisi Zanzibar tumeshamaliza kazi,” alisema Maalim Seif na kushangiliwa na umati wa wafuasi hao.
Hali ilivyokuwa
Mapema kabla ya Lowassa hajawasili Buguruni wafuasi wa CUF walianza kujikusanya taratibu saa 4 asubuhi kwa kuzunguka na ngoma barabara za Uhuru na za mitaa kuingia ofisi za chama hicho.
Baadaye umati huo uliongezeka kiasi cha kufunga barabara ya Uhuru kwa muda wakati Lowassa anaingia saa 6:20 mchana na kupokelewa na Maalim Seif, Makaidi, Mbatia na viongozi waandamizi wa Ukawa.
Idadi hiyo ya watu iliwapa kibarua maofisa usalama wa Ukawa walioonekana wakihaha kutengeneza njia ili viongozi hao wapite.
Baada ya viongozi hao kuwahutubia wafuasi hao, waliingia katika ukumbi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi saa 7:15 mchana na kufanya mazungumza ya takriban saa moja na baadaye viongozi kutoka nje ya CUF kuondoka.
Nafasi ya Lipumba
Kikao cha Baraza Kuu kilijadili nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa na Profesa Lipumba na suala hilo liliachiwa Mkutano Mkuu wa chama ambao utaitishwa baada ya miezi sita kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kufanya uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akitoa taarifa ya kikao hicho, Maalim Seif alisema Baraza Kuu limeunda kamati maalum ya watu watatu itakayofanya kazi na katibu mkuu kwa miezi sita kabla ya Mkutano Mkuu kukaa na kumchagua mwenyekiti na makamu wake, nafasi ambazo ziko wazi.
Waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Twaha Taslima ambaye ni mwenyekiti na wajumbe wawili ambao ni Aboubakary Khamis Bakary (Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar) na Sererina Mwijage (mbunge mstaafu wa viti maalumu.

Hotuba ya Lowassa kujiunga Chadema

Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa akionyesha
Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa akionyesha kadi yake ya uanachama wa Chadema baada ya kujiunga rasmi Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Ndugu waandishi wa habari na ndugu Watanzania wenzangu.
Yamepita majuma mawili tangu mchakato wa kuchagua mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ukamilike. Nimetumia muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika siasa nchini. Ninajua marafiki wengi na wananchi wenzangu wanaoniunga mkono wamekuwa wakisubiri kwa hamu nitoe kauli.
Nilipokuwa natangaza nia ya kugombea urais kule Arusha, nilieleza nia yangu ya kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya nchi yetu na kuondokana na umaskini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma, azma hii bado iko palepale.
Lakini nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa sisi pumzi ya kuendelea kuwa wazima wa afya njema hadi hivi sasa. Nawashukuru pia mke wangu Regina, wanangu, wanafamilia na marafiki wote kwa mapenzi, msaada na uvumilivu wao wakati wa kipindi hiki kigumu tunachopitia. Nawashukuru sana pia maelfu ya wanachama wa CCM walionidhamini na mamilioni zaidi walioniunga mkono.
Katika safari zangu za mikoani wakati wa kuomba udhamini, nilitiwa hamasa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuniunga mkono.Aidha, ninawashukuru sana wana kamati wangu, makundi mbalimbali na mamilioni ya vijana wakiwamo; “For You Movement”, “Friends of Lowassa” “Team Lowassa”, Umoja wa Bodaboda na wengine wengi ambao walijitolea kwa hali na mali katika Safari yetu ya Matumaini.
Nitakuwa sijahitimisha orodha ya shukrani iwapo nitaacha kuwashukuru viongozi wa dini zote nchini ambao waliungana na waumini wao wengi katika maombi na kwa kuniunga mkono. Najua sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea matokeo yale.
Kama ilivyokwishaelezwa, mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.
Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea Urais kupitia CCM.
Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM. Aidha, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM. Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa majungu na uongo mwingi, kuhakikisha kuwa jina langu halifikishwi mbele ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika kuwa nilikuwa mgombea anayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa CCM kuliko wenzangu wote. Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu.
Ni dhahiri kwamba njama dhidi yangu ndani ya CCM si jambo jipya.Kumekuwa na mkakati wa siku nyingi wa kulichafua jina langu kwa uzushi na uongo usio na kifani. Aidha, mmeshuhudia jinsi vijana kadhaa walivyotumika kunikashifu na kunitukana na bila aibu na uongozi wa CCM na Serikali kuwazawadia madaraka makubwa.
Kwa namna ya kipekee napenda kuwapongeza na kuwashukuru wazee wetu akiwamo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na baadhi ya  wajumbe wa Kamati Kuu ikiwa ni pamoja na waheshimiwa Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Alhaj Adam Kimbisa kwa uadilifu na ushujaa wao mkubwa wa kuisimamia katiba ya CCM na misingi ya haki na kukataa maamuzi batili ya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu kuhusu uteuzi wa wagombea.
Cha msingi kuzingatia ni kuwa ili kuhitimisha njama za kunipora mimi na wagombea wengine haki zetu za msingi za kusikilizwa, viongozi wachache walikuwa tayari kupanda mbegu ya chuki na mfarakano ambao ni mfano mbaya kwa CCM na hata Taifa letu. Watanzania walitarajia chama kinachoongoza nchi kiwe ni mfano wa utawala wa sheria na kinara katika kutetea misingi ya haki na demokrasia na siyo kuihujumu. Yaliyotokea Dodoma yameitia dosari nchi yetu.
Kwa kifupi, ninaamini sikutendewa haki katika mchakato mzima wa kupendekeza majina na kuteua mgombea wa urais kupitia CCM. Nilinyimwa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kuchaguliwa.
Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na uadilifu.
Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na SASA BASI!
Kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyosema, CCM siyo baba yangu wala mama yangu na kwamba kama Watanzania hawapati mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute mabadiliko nje ya CCM.
Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya kweli ya nchi yetu. Navishukuru vyama vyote vya siasa chini ya Ukawa, yaani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa mwaliko wao na imani yao na kuthamini mchango ninaoweza kutoa kufanikisha azma ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kweli ya Taifa letu. Waheshimiwa Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, Mheshimiwa James Mbatia na Emmanuel Makaidi asanteni sana.
Ndugu zangu, sikuufanya uamuzi huu kwa pupa, lakini unafika wakati wa kuchukua maamuzi hata kama ni magumu  kwa kuamini fika kuwa ni kwa masilahi ya Taifa letu.
Nimejiridhisha kuwa ndani ya Ukawa Taifa letu linayo fursa ya pekee na ya kihistoria kushinda Uchaguzi Mkuu ujao na ya kuleta mabadiliko ya msingi katika nchi yetu. Kwa uamuzi na ushiriki wangu huu, ninaamini kwa dhati kuwa tutaondoa uhodhi wa madaraka wa chama kimoja na kujenga demokrasia yenye ushindani wa kweli kisiasa.
Namalizia kwa kutoa wito kwa Watanzania wenye nia njema na nchi yetu na wanaotaka kujenga demokrasia na kuleta mageuzi na maendeleo ya kweli, kujiunga nasi katika safari hii mpya ya kuinusuru nchi yetu.
Safari ya Matumaini inaendelea kupitia Ukawa lakini haitafanikiwa iwapo sote hatutajiandisha kupiga kura. Natoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam, kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kwa wingi.
Aidha, nawakumbusha Watanzania kote nchini waliojiandikisha kutunza shahada zao na kukumbushana kupiga kura ili ifikapo Oktoba mwaka huu tupate ushindi wa kishindo.
Ndugu zangu Watanzania, tuungane pamoja kuuondoa umaskini na kuleta mabadiliko ya kweli.
NARUDIA CCM SIYO MAMA YANGU

Pichani kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Mh James Mbatia, Mwenyekiti wa CHADEMA Mh Freeman Mbowe, Waziri mkuu mstaafu Mh Edward Lowassa na Mwenyekiti wa CUF Prf Ibrahimu Lipumba
Pichani kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Mh James Mbatia, Mwenyekiti wa CHADEMA Mh Freeman Mbowe, Waziri mkuu mstaafu Mh Edward Lowassa na Mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahimu Lipumba
Waziri Mkuu mstaafu Mh Edward Lowassa leo amejiunga na Ukawa kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema katika hafla iliyohudhuriwa na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.
Hafla hiyo ambayo imehudhuriwa na Viongozi wote wanaunda umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa akiwemo mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CHADEMA Mh Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Mh James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD Mh Emmanuel Makaidi.
Mh Freeman Mbowe akimkabidhi kadi ya Kujiunga na CHADEMA mama Regina Lowassa
Mh Freeman Mbowe akimkabidhi kadi ya Kujiunga na CHADEMA mama Regina Lowassa
Waziri Mkuu mstaafu Mh Edward Lowassa na Mkewe mama Regina Lowassa wakionyesha kadi zao za Uanachama wa CHADEAMA mara baada ya kujiunga na CHADEMA katika hafla iliyofanyika Bahari Beach Hotel
Waziri Mkuu mstaafu Mh Edward Lowassa na Mkewe mama Regina Lowassa wakionyesha kadi zao za Uanachama wa CHADEAMA mara baada ya kujiunga na CHADEMA katika hafla iliyofanyika Bahari Beach Hotel
Waziri Mkuu mstaafu Mh Edward Lowassa akiwa na Mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahimu Lipumba
Waziri Mkuu mstaafu Mh Edward Lowassa akiwa na Mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahimu Lipumba
Mwenyekiti wa Baraza la wanawake CHADEMA na Mbunge wa Kawe Mh Halima Mdee akisikiliza kwa makini yaliyokuwa yakijili katika hafla ya kujiunga na Chadema kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mh Edward Lowassa
Mwenyekiti wa Baraza la wanawake CHADEMA na Mbunge wa Kawe Mh Halima Mdee akisikiliza kwa makini yaliyokuwa yakijili katika hafla ya kujiunga na Chadema kwa Waziri Mkuu Mstaafu Mh Edward Lowassa
Lowassa ambaye aliambatana na mkewe Mama Regina Lowassa wote walikabidhiwa kadi ya kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mh Freeman Mbowe.