Saturday, October 20, 2012
Waandamanaji 53 mbaroni,baadhi wapenya na kutinga Ikulu
picha zikiwaonyesha waandamanaji waliodhibitiwa.....
Magari ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) yakiwa yamepakia wanajeshi tayari kukabiliana na waandamanaji wa Kiislamu eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam jana.
Jiji la Dar es Salaam jana lililipuka hata kulazimika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuingilia kati na kuongeza nguvu kudhibiti vurugu kubwa zilizotikisa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, zilitokana na maandamano ya baadhi ya waumini wa Kiislamu waliokuwa wanataka kwenda Ikulu.
Magari kadhaa ya JWTZ yaliyosheheni askari wa jeshi hilo yaliranda katika mitaa mbalimbali ya jiji na eneo la Wizara ya Mambo ya Ndani na Ikulu huku helkopta ya polisi ikiwa angani kufuatilia usalama wa eneo hilo.
Askari wa JWTZ waliingilia kati kusaidia jeshi la polisi lililoonekana kuzidiwa nguvu baada ya waandamanaji hao kupambana na polisi hao kwa kuwarushia mawe.
Askari hao waliokuwa na silaha, ikiwemo mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na risasi za moto, walitanda katika maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.
Maandamano na vurugu hizo zilisababisha shughuli mbalimbali hasa biashara na usafiri kusimama huku wafanyakazi wa maeneo ya mjini kuondoka mapema maofisini.
Waumini hao waliandamana kuishinikiza serikali imuachie huru Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislam Tanzania Sheikh Issa Ponda, aliyefunguliwa mashtaka ya uchochezi pamoja na waumini wengine kadhaa walioko mahabusu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, pamoja na Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadik, kwa nyakati tofauti waliwasihi waumini kutawanyika mara baada ya kumaliza ibada ya Ijumaa jambo ambalo baadhi ya Waislam hawakuliafiki.
Askari wa JWTZ hawakujihusisha na kamata kamata ama kupambana na waandamanaji moja kwa moja lakini walikuwa nyuma ya polisi kuhakikisha kuwa pale nguvu inapopungua wanaingilia .
Pamoja na askari wa JWTZ, Vikosi vya Kutuliza Ghasia (FFU), vikishirikiana na askari wa vikosi vya mbwa pamoja na wanamgambo wa jiji walikabiliana na maandamano yaliyoanza baada ya swala ya Ijumaa.
KUPAMBANA NA WAANDAMANAJI
Katika vurumai hizo polisi walitumia virungu, mabomu ya machozi, maji ya kuwasha huku wengine wakiwa na bunduki na risasi za moto kuwatawanya waandamanaji ambao walijibu kwa kuwarushia mawe na vitu vingine.
Licha ya kuwa na vurumai hizo gari la polisi lilitoa tangazo kwa wanausalama kufanya kazi yao kwa tahadhari na kukataza ukamataji watuhumiwa na kudhibiti vurumai usitumie risasi za moto na mabomu ya machozi yaliyokuwa yanarushwa yasielekezwa kwa raia.
Kadhalika polisi waliuzingira msikiti wa Idrisa ulioko karibu na kituo cha Polisi cha Msimbazi kufuatia idadi kubwa ya waandamanaji kukimbilia humo. Ili kuwatoa waliokuwa mafichoni polisi walimwaga maji ya kuwasha ili kuwatoa waandamanaji walioingia ndani kwa kuruka ukuta.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wametanda barabarani hali iliyosababisha barabara kadhaa zikiwemo za Kariakoo, Kinondoni, Kawawa na Morogoro kufungwa.
Mathalani watu walishindwa kupita kwenye barabara ya Kinondoni inayoungana na ile ya Kawawa kutokana na polisi kudhibiti maandamano hayo na kusababisha njia hiyo isipitike.
KARIAKOO YALIPUKA
Kariakoo, ambayo kiuchumi ni kitovu kikubwa cha biashara za Tanzania jana ilizizima kwa moshi na kelele za mabomu na kusababisha biashara za mabenki, maduka ya fedha, soko kuu la vyakula na bidhaa za walaji kufungwa kwa muda wote.
Pia ofisi na vioski zinapouzwa bidhaa na huduma mbalimbali vilifungwa kwenye sehemu nyingine za mitaa ya katikati ya jiji zilizohofiwa kukumbwa na vurumai hizo.
Eneo hili halikuwa shwari kwani wananchi wakiwemo wanafunzi walijikuta katika wakati mgumu huku wangine wakipigwa na mgambo wa jiji na kuishia mikononi mwa polisi wa FFU.
Uharibifu wa mali ulitikisa kwa kuchoma matairi katikati ya barabara pamoja na wezi kupora kwa urahisi bidhaa zilizokuwa maeneo ya wazi.
NIPASHE iliyokuwa eneo la tukio, ilishuhudia malori ya polisi yenye namba PT 18448 , PT 2093, PT 1145 na T662 APM yakiwa yamebeba watuhumiwa na gari la makachero wa upelelezi yakisomba watu kadhaa waliokamatwa kwenye vurumai hizo na kuwapeleka kituo cha Msimbazi .
Walioshikiliwa watabakia rumande hadi Novemba Mosi wakisubiri maamuzi ya hatua zitakazochukuliwa. Kadhalika polisi walifanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kuwakamata waliokuwa wanapambana nao wakiwa majumbani.
TISHIO LA MAISHA
Wakati huo huo vurugu hizo zimesababisha mwanamke mmoja ambaye hakufahamika kuzirai na kupoteza fahamu kufuatia milipuko ya mabomu ya kutoa machozi iliyorindima Kariakoo.
WANANCHI WALAANI
Watu mbalimbali wamelaani tukio hilo na kuitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanaosababisha vurumai kwani zinahatarisha amani ya nchi
Kwa upande wake, Skeikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Sheikh Alhadi Salum aliwaomba Waislamu kuacha kuandamana na kwamba waliache sheria ichukue mkondo wake na suala la dhamana ni haki ya kila mmoja, hivyo watapatiwa.
Viongozi wa dini walitoa wito wa kutafuta suluhu kwa kuaa pamoja ili kufikiana muafaka.
KOVA ALONGA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, akizungumzia vurumai za jana alisema hakuna polisi wala raia aliyepoteza maisha jana.
Kova aliongeza kuwa waliokamatwa ni kutokana na vurugu hizo ni 53 na kwamba walitiwa mbaroni baada ya kukaidi amri ya serikali ya kuwataka wasiandamane . Katika hatua nyingine alisema waliojeruhiwa ni wale waliokimbia ovyo.
Alisema hakuna risasi zilizotumika mbali na mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kudhibiti vurugu hizo.
NCHIMBI ATETA NA VIONGOZI WA ULINZI
Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchimbi, jana alikutana na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wa wizara hiyo. Habari tulizozipata kabla ya kwenda mitamboni zilisema.
JK ATOA POLE
Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema kuomboleza kifo cha askari polisi Said Abdulrahman aliyuawa kikatili visiwani Zanzibar.
Abdulrahman wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), aliuawa kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi usiku wa Jumatano wiki hii katika eneo la Bububu wakati akirejea nyumbani baada ya kazi kazi.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kuuawa kikatili kwa askari wetu Said Abdulrahman wa kikosi cha Kutuliza Ghasia usiku wa tarehe 17 Oktoba wakati akirejea nyumbani kwake, baada ya kukamilisha zamu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao kwa siku hiyo,” alisema Rais Kikwete.
“Kitendo hiki cha mauaji ni kitendo kiovu, ni cha kikatili na kinachostahili kulaaniwa na kufanyiwa kila aina ya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo,” alisema Rais Kikwete katika salamu hizo.
Alisema anaungana na familia hiyo kumwomba Mwenyezi Mungu, ailaze roho yake mahala pema peponi .
HOSPITALI YA AMANA
Majeruhi tisa wa vurumai hizo walifikishwa katika hospitali ya Amana ambapo nane kati yao walitibiwa na kuruhusiwa wakati mmoja Neema Samson (26) amelazwa.
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment