Dk Mwakyembe |
Ni takribani wiki ya tatu sasa tangu wasichana wawili wa Tanzania walipokamatwa na kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 6.8 nchini Afrika Kusini wakati zikisafirishwa kutoka Tanzania.
Jana NIPASHE lilizu ngumza na Dk. Mwakyembe kwa njia ya simu kutoka Kagera, lakini alijibu kwamba, hana taarifa za kina kuhusu sakata hilo.
Hata hivyo, alisema yeye hausiki nalo kwa kuwa suala la uhalifu linaihusu Polisi na kumwelekeza mwandishi awasiliane na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi au Jeshi la Polisi.
Taarifa za kukamatwa kwa wasichana hao nchini Afrika Kusini zilipatikana Julai 5, mwaka huu. Walikamatwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato ya nchi hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, uliopo eneo la Kempton Park.
Taarifa hiyo ilionyesha wasichana hao walisafirisha dawa hizo kupitia ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini.
Waliokamatwa hivi karibuni ni Agnes Jerald (25), Melisa Edward (24), ambao wameshtakiwa Afrika Kusini.
Hata hivyo, kigugumizi cha viongozi hawa na hususan cha Waziri Mwakyembe, kinaibua maswali mengi, ambayo yanaashiria kwamba, biashara haramu ya dawa za kulevya itakuwa inahusisha mtandao wa watu wenye nguvu nchini.
Itakumbukwa kwamba, ni Mwakyembe huyu huyu, ambaye aliifumua Mamlaka ya Bandari (TPA), kwa kuwatimua kazi wakurugenzi wakuu pamoja na kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi kutokana na utendaji usio na tija na hasa baada ya kutokea kwa wizi wa shaba bandarini.
Wizi huo ulitokea usiku wa kuamkia Septemba 8, mwaka jana jambo, ambalo lilimkasirisha Waziri Mwakyembe.
Alifanya ziara bandarini hapo na kuagiza watu wote waliohusika na wizi huo kukamatwa na kufunguliwa mashitaka.
Pia Juni 12, mwaka jana, Mwakyembe baada ya kuwang’oa vigogo wanne wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), alisafiri kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ili kujionea utendaji kazi wa shirika hilo. Mara baada ya kuwasili katika Stesheni ya Dodoma saa 1:30 asubuhi, alizungumza na waandishi wa habari na kusema akiwa katika safari hiyo, alipata fursa za kutembelea mabehewa yote na kuzungumza na abiria. Alisema alibaini hujuma nzito katika Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), ikiwamo ofisa mmoja kuwaibia abiria kwa kughushi viwango vya nauli na hivyo akaagiza afukuzwe kazi.
Licha ya kuagiza kutimuliwa kwa ofisa huyo, pia alitangaza kuandaliwa utaratibu wa kufanya mabadiliko kadhaa katika kuboresha usafiri huo, ikiwamo kuondoa malipo ya nusu nauli kwa watoto wadogo kuanzia miaka mitatu hadi miaka 10 na pia kuondolewa kwa utaratibu wa malipo ya mizigo midogo ya abiria.
Takwimu zinaonyesha kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na dawa hizo.
chanzo...gazeti la nipashe