Matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012, yameendelea kuitikisa sekta ya elimu nchini baada ya shule kufunguliwa jana bila kutangazwa kwa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.
Kwa kawaida, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na
vyuo vya ualimu, hutangazwa mapema ili kutoa fursa kwa wanafunzi na
shule husika kufanya maandalizi ya mahitaji.
Lakini tofauti na ilivyozoeleka, wanafunzi wa kidato cha sita
walianza masomo yao jana huku wale wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha
tano na vyuo vya ualimu wakiwa hawajatangazwa.
Mkanganyiko huo pia unazigusa shule za sekondari za binafsi kwani
baadhi zilishachukua wanafunzi wa kidato cha tano na nyingine
ziliahirishwa kufunguliwa jana kutokana na kutokuwa na wanafunzi hao.
Hali hiyo imewaacha njia panda baadhi ya wakuu wa shule ambao
waliwaambia waandishi wetu kwa nyakati tofauti kwamba wanasubiri
maelekezo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu suala hilo,
huku wengine wakitishia kufunga shule hizo na kuzigeuza kuwa vyuo vya
taaluma nyingine.
Akitangaza matokeo mapya ya kidato cha nne Mei mwaka huu, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliahidi kwamba majina
ya watakaojiunga na kidato cha tano yangetangazwa mapema ili wapate muda
wa kujiandaa na kuripoti kwenye shule husika mapema kadri
itakavyowezekana.
Jana, Dk Kawambwa hakupatikana kuzungumzia suala hilo na msemaji wa
Wizara hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema suala la kutangaza majina hayo lipo
kwenye ngazi za uamuzi.
“Sababu hasa siwezi kujua, lakini kwa kuwa matokeo yenyewe
yalichelewa kutangazwa ni rahisi hata mchakato wa kutangaza
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano uchelewe,” alisema Bunyanzu.
Wakuu wa shule
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Morogoro, Thomas Chihwalo alisema: “Ninachosubiri ni maelekezo ya wizara, nini kifanyike.”
Mkuu wa Sekondari ya Azania, Dar es Salaam, Benard Ngoyaye
alipoulizwa alisema: “Nenda kwa Ofisa Elimu wa Wilaya, yeye anafahamu
kwa nini majina yamechelewa kufika wakati walikwishachaguliwa.” Mkuu wa
Shule ya Sekondari Arusha, Christopher Malamusha alisema walitarajia
wizara ingetangaza majina hayo mapema lakini hadi jana walikuwa
hawajapokea taarifa zozote.
Mkuu wa Sekondari ya Tambaza aliyejitambulisha kwa jina moja, Zuberi
naye alisema wanasubiri maelekezo ya Ofisa Elimu Wilaya ya Ilala.
Hata hivyo, Ofisa Elimu ya Sekondari wa Manispaa ya Ilala, Germana
Mng’aho alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo na kwamba mhusika mkuu
ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Mkuu wa Shule ya Sekondari ya
Ilboru, Arusha, Julius Shula alisema hata majina ya wanafunzi
wanaojiunga na shule yao hawayafahamu.
Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani, Dar es Salaam,
alisema kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano huripoti shuleni wiki
mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu ambacho mwaka huu kimekuwa
tofauti. Msaidizi wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwiru Wavulana ya
Mwanza, Malongo Charles alisema wanasubiri wanafunzi watakaopelekwa na
Serikali.
Hata hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Moshi, Fanuel Angalo alisema anaamini wizara husika itatangaza wiki hii.
“Ni jambo jipya kidogo limetokea lakini tunaamini Waziri atatoa
tangazo lake wiki hii halafu wanafunzi hao wa kidato cha tano waripoti
shuleni wiki ijayo,” alisema Angalo.
Mkoani Tanga, walimu katika Shule za Sekondari za Tanga Ufundi,
Gallanos na Usagara kwa nyakati tofauti, waliilalamikia wizara kwa
kuwachelewa kuwapelekea wanafunzi wa kidato cha tano na kusema kuwa hiyo
imevuruga utaratibu wa ufundishaji.
Hakuna athari
Baadhi ya wadau wa elimu walisema kilichotokea si kigeni kwani
kimepata kutokea miaka ya nyuma na mihula ilirekebishwa na kwenda sawa
na wenzao ambao walikuwa wameanza masomo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Ushauri wa HakiElimu, Nyanda Shuli
alisema kubadilika kwa muhula wa kuanza masomo si jambo kubwa ambalo
linaweza kuathiri elimu na kwamba anaamini wizara itakuwa imetoa
mwongozo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila
Mkumbo alisema si mara ya kwanza kwa muhula wa masomo kubadilika kwani
imewahi kutokea siku za nyuma na marekebisho yakafanywa ili kufidia muda
ambao wanafunzi wanakuwa wamepishana na wenzao.
“Sidhani kama ni jambo kubwa sana ambalo linaweza kuathiri chochote
katika masuala ya elimu, la msingi ni kuhakikisha kuwa waliochelewa
kuanza masomo wanapata muda wa kumaliza mtaala (mtalaa) wa masomo kama
inavyotakiwa.”
Kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Juni 29, mwaka huu, wakuu wa shule
za sekondari za Serikali walikutana katika Chuo cha Ufundi, Arusha
kupitia majina ya waliochaguliwa na kuiachia kamati ya kukamilisha kazi
hiyo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema tatizo kubwa
lilikuwa ni idadi ya wanafunzi kuwa ndogo ikilinganishwa na nafasi za
kidato cha tano kutokana na kufeli kwa wanafunzi wengi katika matokeo ya
kidato cha nne, 2012.
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment