WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amewataka
waandishi wa Habari wa kike kutumia kalamu zao katika kuandika mambo
yanayohamasisha amani na utulivu nchini.
Pia aliwataka kutumia kalamu zao katika kuandika na kuibua vitendo vya
unyanyasaji na vya kikatili wanavyofanyiwa wanawake nchini.
Hayo aliyasema hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika Hotel ya Lamada , wakati
wa uzinduzi wa kikundi cha Habari Group kinachojumuisha waandishi
mbalimbali wa habari hapa nchini.
Alisema ni vyema wakatumia fursa zao katika kufichua viashiria
mbalimbali vya fujo kwa kuwa endapo itatokea uvunjifu wa amani
wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto.
Kikundi cha habari kinajihusisha na ununuaji wa hisa, kukopeshana na
kufanya miradi mbalimbali ya kikundi na mmoja mmoja hivyo aliwataka
wanakikundi kujibidiisha zaidi na kuongeza wanachama wake.
“Uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ni moja ya maadhimio 12 ya ulingo wa
Belgin hivyo mnachofanya hapa ni katika kujikwamua wenyewe kiuchumi na
kama mnavyofahamu wanawake wanamajukumu mengi katika familia na pia
kutingwa na mambo mengi katika tasnia yenu lakini mmethubutu kufanya
hivyo hivyo endeleeni,”alisema Kagasheki
Pia alitoa wito kwa wanawake kuhakikisha kuwa majukumu waliyonayo yasiwe kikwazo kwao kushiriki katika kukuza uchumi.
Alisema kinachotakiwa ni kuondoa fikra kuwa haiwezekani na kuhakikisha
wanapiga vita mambo yanayomgandamiza mwanamke kwa kuondoa fikra kwamba
haiwezekani kujikwamua kiuchumi.
Naye mlezi wa kikundi hiko ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Angella Kairuki alisema atakuwa bega kwa bega na wanakikundi hiko
katika kuhakikisha kuwa kinasonga mbele.
“Nimefurahishwa sana na wazo la wanahabari hawa na nina ahidi nitakuwa
nao bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa kikundi kinakua zaidi na
kuwatafutia fursa mbalimbali za kukiendeleza pia,”alisema Kairuki.
Naye Meneja Uhusiano wa PPF Lulu Mengele alisema wamekuwa katika mstari
wa mbele katika kutoa mikopo kwenye saccos nchini kwa wanachama wao
sehemu za kazi.
Alisema tayari wametoa mikopo kwa wanachama wake kwenye maeneo ya kazi
41 yenye thamani sh bil 48.7 lengo likiwa ni kumsaidia mwanachama akiwa
kwenye ajira.
Aliendelea kueleza kuwa PPF inachukua jukumu la kusomesha watoto wa
wanachama ambao wazazi wao wamefariki kuanzia chekechea hadi kidato cha
nne ambapo kwa sasa tayari wanasomesha 1333 katika shule mbalimbali.
Alisema PPF inatoa mafao saba ambapo aliyataja kuwa ni pamoja na
uzee,ugonjwa,kiinua mgongo,kifo ,elimu,kujitoa, sambamba na kuandikisha
wanachama kutoka kwenye sekta mbalimbali na kupata taarifa zaidi kupitia
simu ya mkononi.
Naye mratibu wa kikundi cha habari group Rabia Bakari akisoma risala
mbele ya mgeni rasmi alisema kikundi kinahitaji zaidi ya milioni 10 ili
kila mmoja
aweze kupata mkopo kwa wakati bila kupeana kwa zamu ili kuharakisha shughuli za maendeleo.
”Kwa sasa katika akaunti yetu tumefanikiwa kuwa na milioni mbili na nusu
tu, hivyo tunahitaji zaidi ya milioni 23 ili kufanikisha malengo
tuliyojiwekea,”alisema Rabia.
Mara baada ya mgeni rasmi kuzindua kikundi kulifanyika harambee ambapo
zilichangwa zaidi ya sh mil 6 ambapo mgeni rasmi alitoa mil 2 na mama
mlezi wa kikundi alitoa 1.5 mbunge wa Busega Dk.Titus Kamani alitoa laki
2, Jumuia ya kukuza uchumi Ilala laki sita ,TAMADA laki 2 pamoja na
wadau wengine
No comments:
Post a Comment