Friday, June 5, 2015

Urais CCM: Makada 10 waingia uwanjani.

Lowassa aahidi neema watumishi wa CCM, Bilal asema atarejesha miiko ya uongozi, Magufuli: Nitasimamia Ilani ya chama, Sumaye asisitiza atakufa na walarushwa.
Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chao kuwania urais huku Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akiweka msimamo kwamba anaingia kwenye mbio hizo akiwa na matumaini ya kushinda na siyo kushindwa.
 
Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na mmoja wa waandishi wa habari kama CCM haitampitisha je, atakuwa tayari kumuunga atakayeteuliwa?
 
“Sina mpango wa kushindwa,” alisema bila kufafanua katika hadhira iliyokuwa imejaa waandishi na wafuasi wa CCM kwenye Makao Makuu ya chama hicho mjini Dodoma jana.
 
Mbali na Lowassa wengine waliochukua fomu jana ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, Balozi Ali Karume, Mfanyakazi wa CCM Idara ya Uhusiano na Siasa, Amos Siyatemi na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.
 
Orodha hiyo imefikisha makada wa CCM wanaowania urais kuwa 13. Walikwisha kuchukua fomu ni 10 hadi jana.
 
Lowassa ambaye alikuwa mwanachama wa tano kuchukua fomu kati ya watangaza nia sita kwa siku ya jana, hali ilikuwa tofauti na wagombea wengine kutokana na umati mkubwa wa wananchi kujitokeza wakiwamo wanafunzi wa vyuo vya mjini Dodoma na akina mama wafugaji wa Kimasai.
 
Lowassa aliwasili katika viwanja vya CCM makao makuu Dodoma saa 10:09 jioni akiwa na msafara wa magari zaidi ya manane akisindikizwa na baadhi ya wabunge na wenyeviti wa CCM wa mikoa.
 
Wabunge walioonekana kumsindikiza ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, Naibu Waziri wa Kazi na Vijana, Makongoro Mahanga, Anna Abdallah (Viti Maalum), Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye.
 
Wenyeviti wa CCM mikoa walijitokeza kumsindikiza Lowassa ni, Mgana Msindai (Singida), Khamis Mgeja (Shinyanga), Onesmo Nangole (Arusha), Mohamed Sinaye (Mtwara).
 
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Lowassa alisema katika mbio za kusaka urais mwaka huu hakusudii kushindwa bali kushinda.
 
RUSHWA NA UFISADI
Akijibu swali kwa nini baadhi ya makada wenzake wanamhusisha na vitendo vya wizi na ufisafi, alisema kama kuna anayejiamini amtaje kwa hoja. Alisema amechoka utaratibu wa siasa za tuhuma na matusi ambazo haziwezi kusaidia nchi katika maendeleo na wala hazitaweza kupima viongozi kwa rekodi zao.
 
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli alisema vyombo vya habari visaidie kuwaelimisha wananchi, maana hawezi kujibu kila mtu mambo ambayo hayana maana.
 
"Nimechoka kujibu tuhuma na matusi ya nguoni na kimsingi hizi ni siasa za maji taka, wabaneni watu kwa rekodi zao wewe umefanya nini toka umekuwa kiongozi, tuulizane bila aibu anafanya nini kumtoa Mtanzania na kwa mipango gani na je, kuwa rekodi yake anaaminika au ni bulabula," alisema.
 
Alisema hakuna sababu ya kuchonganishwa kwani hali hiyo haiwezi ikasaidia kupata viongozi waliobora. Alisisitiza kinachotakiwa ni kuwa na mijadala itakayoleta viongozi wanaokubalika na watu.
 
UTEUZI WA BARAZA LA MAWAZIRI
Alipoulizwa iwapo atachaguliwa kuwa rais atawateua watu waliokaribu naye katika Baraza la Mawaziri, alisema hilo litajulikana atakapovuka daraja.
 
Awali alieleza kuwa kama atachaguliwa, ataanza kushughulikia matatizo ya wafanyakazi wa CCM makao makuu ambao wanakimbiliwa na matatizo mengi.
 
"Makao makuu ya CCM ndio roho ya chama, naelewa matatizo yanayowakabili watumishi wa chama kuhusu malipo ya mishahara midogo, hawakopesheki na hawalipwi  fedha za likizo.
 
Alisema Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi nzuri sana kukiimarisha chama na kwamba kinachotakiwa sasa ni kukiimarisha kiuchumi ili kisiwe ombaomba.
 
"Kama chama kitanipa ridhaa ya kuwa rais nitashughulikia matatizo ya watumishi kwani bila CCM madhubuti na bila viongozi wazuri CCM itayumba," alisema.
 
MATESO KWA WANANACHI
Akizungumzia kuhusu mateso wanayofanyiwa wananchi na wanahabari, alitoa pole kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kinanda, na kwamba vitendo wanavyofanyiwa wananchi siyo demokrasia.
 
"Nalaani vitendo hivyo na serikali yangu haitakuwa tayari kuingilia uhuru wa mtu," alisema .
 
MAGUFULI AINGIA MITINI KUZUNGUMZA NA WAANDISHI
Waziri wa Ujenzi, Dk. Magufuli alifunga dimba kwa kuchukua fomu, lakini aliingia mitini kuzungumza na waandishi waliokuwa wakimsubiri katika ukumbi wa CCM makao makuu.
 
Wakati waandishi wakimsubiri ukumbini kwa zaidi ya nusu saa ghafla ofisa habari wa CCM makao makuu, alifika na kuwaeleza kuwa Dk Magufuli ameshachukua fomu na kuondoka zake.
 
AMOS SIYANTEMI; NITAFILISI WALA RUSHWA
Naye Amos Siyantemi wa CCM ambaye ni mtumishi wa chama amechukua fomu na kusema kuwa amefikia uamuzi wa kugombea nafsi hiyo ili kurudisha imani ya chama kwa wananchi na kwamba akichaguliwa atahakikisha anawafilisi wala rushwa.
 
"Vitendo vya rushwa katika chaguzi mbalimbali kunaweza kukiangamiza chama, hivyo atahakikisha kuwa wote watakaotuhumiwa na rushwa watafilisiwa mali zao," alisema Siyantemi.
 
Alisema atahakikisha anarejesha misingi ya azimio la Arusha la ujamaa na kujitegemea.
 
Kada huyo alisema suala la huduma za jamii ikiwamo afya atalipa kipaumbele kikubwa ikiwamo kuhakikisha kuwa badala ya kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kutibiwa atawaleta wataalam hao hapa nchini ili kupunguza gharama za serikali.
 
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye alisema atahakikisha anakomesha suala la wafanyakazi wa umma kuwa wafanyabiashara na kuahidi kuunda vyombo viwili vya kupambana na rushwa.
 
Alivitaja vyombo hivyo kuwa ni chombo cha uchunguzi na mahakama maalum kwa watuhumiwa wote wa rushwa.
"Kila kiongozi au mfanyakazi wa umma lazima achague kati ya biashara au kufanyakazi,” alisema.
 
Sumaye alisema hataki kuwa na vipaumbele vingi bali atakuwa navyo vichache ikiwamo vya kupambana na rushwa.
 
"Ikiwa nitapata ridhaa ya chama changu sitakuwa na mchezo katika kupambana na rushwa kwani matatizo mengi ambayo yapo dawa ni uchumi tu, hakuna mtambo wa uzalishaji wa kuboresha elimu, huduma za afya na mengineyo, lakini mtambo wa yote hayo ni kuwa na uchumi imara," alisema Sumaye
 
DK.BILAL
Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, amesema nia na madhumuni ya kujitokeza kuchukua fomu ya kuwania urais ni kusaidia kuiletea nchi mabadiliko zaidi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Dk. Bilal alisema hatua hiyo ameitumia kama ni haki yake kidemokrasia kama mwanachama na Mtanzania ambaye anaamini ana uwezo wa kulisaidia Taifa kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
 
"Nia na madhumuni ni kukipa uimara zaidi chama chetu maana bila ya kuitikia wito kwa kila mwenye nia na uwezo wa kujitokeza basi nisingekuwa nimekitendea haki chama chetu," alisema Dk.Bilal
 
VIPAUMBELE KATIKA AWAMU YA TANO
Dk. Bilal alisema endapo atapata ridhaa ataendeleza pale walipomalizia wenzake bila kupoteza mwelekeo.
 
"Hivyo ili Taifa letu lizidi kuendelea kutumia fursa ambazo kiongozi wetu Dk. Kikwete ameanzisha kwa kushirikiana nasi naomba niungwe mkono ili niweze kupeperusha bendera ya chama, kupitia sera, malengo na ilani ya CCM na vipaumbele vikuu," alisema Bilal. 
 
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kulinda misingi ya utaifa na kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa imara, lenye upendo na mshikamano.
 
Alisema atahakikisha anaimarisha umoja, utaifa, uhuru, ulinzi na usalama wa Taifa ili kunusuru Muungano.
 
"Muungano siyo kama ulivyo kuwa zamani, sasa unakabiliwa na changamoto nyingi zaidi, kwa hivyo ni jukumu langu kuhakikisha nitashirikisha wadau mbalimbali ili kutatua changamoto hizi na tutaimarisha muungano wetu," alisema
Kuhusu uchumi, Dk. Bilal alisema atahakikisha anashirikisha wananchi kiuchumi ikiwa ni pamoja na kukuza sekta ya viwanda, ujasiriamali na teknolojia, sekta binafsi ambayo ni shirikishi, kilimo, ushirika na ugatuzi wa madaraka kwa wananchi.
 
Alisema madaraka yatagatuliwa katika ngazi za vijiji na vitongoji, na pia kuendeleza kuzalisha ajira mbalimbali ili kuhakikisha wanaboresha maisha ya Watanzania wote na iwe Tanzania shindani katika kanda, Afrika na Dunia kwa ujumla.
 
Aidha alisema katika matumizi ya rasilimali za Taifa atahakikisha anasimamia vyanzo vya mapato na kuhakikisha yanatumika ipasavyo kuleta maendeleo kwa Watanzania.
 
MIIKO NA MAADILI YA VIONGOZI
Dk. Bilal alisema atahakikisha anarejesha na kusimamia maadili na miiko ya uongozi pamoja na utumishi wa umma kutokana na nchi kupoteza maadili, hivyo atasimamia taasisi za umma na uwajibikaji wa mtu mmoja.
 
Alisema atalinda haki za binadamu ikiwa ni pamoja na utawala bora na kuhakikisha nchi inasimamiwa kwa misingi ya sheria.
 
"Awamu ya tano inaendelea kusimamia na kuimarisha utawala wa sheria, haki za binadamu, haki za kina mama na watoto na walemavu hasa wa ngozi, haki ya kuunda asasi za kiraia pamoja na uhuru wa kupata habari," alisema Dk. Bilal
 
BALOZI KARUME
Alisema mtu ambaye siyo mwadilifu asikabidhiwe nchi kwani itakuwa ni hatari kwa nchi.
 
MUHONGO, SITTA, KAMANI ZAMU YAO LEO
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk Titus Kamani na Mbunge wa Kuteuliwa na Rais Prof. Sospeter Muhongo watachukua fomu leo. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment