Friday, September 28, 2012

Waziri wa Utalii Balozi Kagasheki, ndani ya Spain

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki (kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Taleb Rifai katika Makao Makuu ya Shirika hilo mjini Madrid, Hispania
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki (wanne kushoto) akiwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Taleb Rifai (wa tano kushoto) katika Makao Makuu ya Shirika hilo mjini Madrid, Hispania. Wengine katika picha ni wajumbe wa sekretarieti ya shirika hilo pamoja na ujumbe uliofuatana na Waziri Kagasheki.

Na Carren Mgonja
Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UNWTO) Bw. Taleb Rifai amewataka Watanzania kuutumia mkutano ujao wa masuala ya Uhifadhi na Utalii utakaofanyika nchini kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo kwa washiriki wa mkutano huo.

Rifai aliyasema hayo jana mjini Madrid alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki.


Rifai alisema kuwa Tanzania inavivutio vingi vya utalii lakini jitihada za makusudi zinahitajika kuvifanya vifahamike ulimwenguni  na hivyo kuongeza idadi ya watalii nchini ambayo hadi sasa haijafika milioni moja licha ya utajiri wa vivutio vilivyopo na kuongeza kuwa mkutano wa ujao wa masuala ya uhifadhi na utalii utakaofanyika mjini Arusha mwezi ujao ni fursa muhimu kwa nchi yetu kujitangaza ipasavyo

‘Sekta ya Utalii ndiyo yenye matumaini mazuri kwa uchumi wa Tanzania iwapo itatumika ipasavyo kwani itaweza kuongeza idadi ya wageni na hivyo kuongeza pato la taifa pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wengi zaidi’ alisema Rifai.


Kwa upande wake Balozi Kagasheki alisema kuwa serikali imeamua kwa dhati kabisa kuifanya sekta ya utalii kuwa na tija kwa uchumi wa nchi kwa kuweka malengo ya kuwa na idadi ya watalii milioni moja katika muda mfupi ujao na kusema kuwa hilo litafanikiwa kutokana na mikakati mizuri iliyowekwa kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.


Balozi Kagasheki alilitaka shirika la UNWTO kushirikiana vema na serikali ili kuhakikisha kuwa pande zote zinanufaika. Aidha, alipongeza uamuzi wa shirika hilo kuuleta mkutano huo nchini ambao unafanyika kwa mara ya kwanza nchini katika Bara la Afrika na kuahidi kuwa serikali itatoa kila aina ya ushirikiano ili kufanikisha  mkutano huo.


Waziri Kagasheki na ujumbe wake walitembelea Makao Makuu ya UNWTO kwa ajili kuzungumzia masuala mbalimbali ya uhifadhi na utalii nchini hususan mkutano ujao ambao utahusisha washiriki mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali duniani.


Mkutano wa First Pan African Conference utafanyika mjini Arusha kuanzia tarehe 15-18 mwezi ujao na utalenga katika masuala ya changamoto na fursa zilizopo katika eneo la utalii endelevu na uhifadhi kwa lengo la kuangalia namna uhifadhi na utalii unavyoweza kufanya kazi kwa pamoja bila kuathiri upande wowote.

No comments:

Post a Comment