Monday, September 3, 2012

Jaribio la Kuuwawa kwa Kiba ni 'sinema'?

KAMA unavyojua, ulimwengu wa mastaa wa Kibongo haukosi jambo ndiyo maana kila leo, heri ya jana. Wiki iliyopita upepo ulivuma kutokea kwa ‘malejendari’ wa Bongo Fleva, Khaleed Mohamed ‘TID’ na Ali Saleh Kiba na kuibua sinema nyingine mpya kwenye sanaa yetu.



Habari ilikuwa hivi; TID au Top In Dar au Mnyama kama anavyojiita, alishikiliwa na polisi katika Kituo Kikuu cha Kati (Central), Dar baada ya kutuhumiwa kupanga njama za kumuua Kiba.
Kwa mujibu wa meneja wa Kiba aliyetajwa kwa jina moja la Gonga, walipata ujumbe unaosema kuwa kuna watu waliokuwa wametumwa nyumbani kwa Kiba Kariakoo, Dar ili kumuua.
Akafafanua kwamba baada ya taarifa hizo kufika kwenye familia, waliamua kuripoti ishu hiyo polisi ambao walifika pale nyumbani na kukuta mwanamke na mwanaume, ambao walifika maeneo jirani, wakawa wameweka kambi kwa muda wakijaribu kuchunguza hili na lile.
Jamaa akaweka wazi kuwa baada ya watu wa karibu kuwaona na kutowatambua, polisi waliamua kuwafuatilia na kuwaweka chini ya ulinzi kisha kuwapeleka kituoni.
Walipowahoji kwa takribani saa nane, wakakiri kuwa walikuwa wametumwa kufanya tukio hilo baya kwa Kiba na kwamba siyo wenyeji wa Dar ila wametokea mikoani.
Walipobanwa nani aliyewatuma, wakamtaja TID, basi moja kwa moja polisi wakaenda kumkamata Mnyama na kushikiliwa kituoni kwa mahojiano.
Pia kuna madai kuwa kabla ya kuanza kumuwinda Kiba, inasemekana TID na watu hao walikutana kwenye nyumba moja huko Mtoni-Kijichi, Dar na kupanga mpango huo.
Kwa upande wake, TID alikana kujua chochote juu ya sakata hilo huku akiweka wazi kuwa Kiba ni mtu wake na tangu azaliwe hakuwahi kufikiria jambo hilo.
Baada ya kusikia kilichojiri hebu tuwaweke TID na Kiba kwenye mizani yetu kupima madai hayo kama ‘yana-sound’.
Nimewafuatilia TID na Kiba wakikua kimuziki na sasa wana takribani miaka 10 japo TID anamzidi Kiba kwa ukongwe kwenye gemu na umri.
Wote wamekuwa wakigonga shoo kubwa za ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, wakati sakata hili linaibuka, TID alikuwa akitokea Afrika Kusini na Kiba alitokea Denmark kwenye shoo.
 Mwaka jana tulishuhudia TID na Kiba wakipiga bonge la shoo nchini Uingereza na hata ukiniamsha usiku wa manane nitakuambia kuwa TID na Kiba ni marafiki mno kama alivyosema Mnyama.
Kwa nini TID? Kwani tatizo ni nini hadi afikie hatua hiyo? Wamezidiana kibiashara?
Wanagombea wanawake kwa sababu wote ni sukari ya warembo? Kuna siri gani nyuma ya pazia?
Maswali hayo hayajibiki hapa kwa sababu ishu hiyo inafanyiwa upelelezi hivyo naamini majibu yatapatikana tu.
Kama kawaida huwa tunajaribu kulitazama jambo kwa namna ya tofauti na hicho ndicho nilichokifanya kwamba kuna madai kuwa sakata hili ni la kutengeneza ili kuwarudisha kwenye gemu wahusika ambao wamefifia kisanaa.
Kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa ili kurudi kwenye gemu kwa kishindo lazima kuwe na skendo lakini siamini hivyo kwani kazi nzuri ndiyo inayomrudisha mtu kama amefifia au amepungua mguso kwenye jamii.
Nasema hivyo kwa sababu nina uzoefu na mastaa wetu ambao hawajui kuwa kurudi kwa mtu kunategemea na ukaribu uliopo kati yake na jamii. Sitaki kuzungumzia ile skendo ya TID kwa watoto yatima wa Kituo cha Maunga Centre, Kinondoni, Dar.
Hata hivyo, mara kadhaa TID amekuwa akisema kuwa ushindani kwenye gemu na kuibuka kwa vijana wapya wanaopata mafanikio ghafla kama akina Nasibu Abdul ‘Diamond’ huwa inamjengea picha kuwa wao (yeye na wakongwe wenzake) wamefanya kazi kubwa ya kujenga msingi imara wa muziki wa Bongo Fleva hivyo hana chuki katika hilo na yupo tayari kuwasapoti. Sasa hili jipya limekujaje? Nahisi kuna sinema tena ya Kihindi. Tusubiri matokeo!  habari na picha kwa hisani ya gazeti la ijumaa wikienda

No comments:

Post a Comment