Friday, December 4, 2015

Waziri Mkuu Majaliwa afanya ziara ya kushtukza TRL


 
Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Shirika la Reli (TRL) na kukagua mabehewa yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye stesheni hiyo ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya michango ya wafanyakazi.


Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi Elias Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha sh. bilioni 13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo. “Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha kibiashara lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.


“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh. bilioni 3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala ya kufanya miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui mnarudishaje huo mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu.


Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL, Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo ya kuanzia Julai – Novemba 2014.


Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka Mhandisi Mshana asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa na uhuru wa kuchagua aina ya usafiri wautakao.

“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema.

No comments:

Post a Comment