Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru
Kawambwa (kushoto), akitangaza matokeo ya mtihani ya Taifa wa darasa
la saba wa mwaka huu mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana. Kulia ni Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalucela.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema jumla ya wanafunzi 560,706 wamefaulu na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali mwaka 2013.
Dk. Kawambwa alisema idadi hiyo ya waliochaguliwa ambayo ni sawa na asilimia 64.78, ni kati ya watahiniwa 865,534 waliofanya mtihani huo mwaka huu na kwamba shule zote za msingi za serikali zipatazo 16,331 zimefanya vizuri katika mtihani huo.
“Shule za serikali zisipewe majina mabaya, kimsingi zimefanya vizuri sana mwaka huu, tuzipe ushirikiano,” alisema Dk. Kawambwa.
Dk. Kawambwa alisema kati ya wanafunzi hao waliochaguliwa mwaka huu, wasichana ni 281,460 sawa na asilimia 50.20 na wavulana ni 279,246 sawa na asilimia 49.80.
Katika matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2011, jumla ya wasichana waliofaulu walikuwa ni 27,377 na wavulana ni 289,190.
Waziri huyo alisema kwa mujibu wa matokeo hayo, idadi ya wanafunzi waliochaguliwa mwaka huu ambayo ni asilimia 64.78 imeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na wanafunzi 515,187 waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka 2011 ambao walikuwa sawa na asilimia 58.28.
Dk. Kawambwa alisema matokeo hayo yanaonyesha kuwa watahiniwa 3,087 walipata alama za daraja la A, wanafunzi 40,683 walipata daraja la B, wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja la C , 526,397 daraja la D na watahiniwa 73,264 walipata daraja la mwisho la E.
Alisema alama ya juu ya kufaulu mtihani huo ilikuwa ni 234 kati ya 250 kwa wavulana na wasichana.
UDANGANYIFU WAPUNGUA
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2012 imepungu kwa asilimia 97 ukilinganisha na mwaka jana.
Dk. Kawambwa alisema katika mtihani kumaliza elimu ya msingi mwaka 2011 watahiniwa 9,736 walifutiwa matokeo baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu wakati mwaka huu waliofutiwa matokeo hayo ni 293 tu.
Waziri Kawambwa alisema kuwa kufuatia udanganyifu huo, serikali itafanya uchunguzi kuwabaini wale wote waliohusika katika udanganyifu na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
WASIOJUA KUSOMA, KUANDIKA WAONYWA
Dk. Kawambwa alisema kuwa wanafunzi waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, atakayebainika hajui kusoma wala kuandika atafutiwa usajili na kupelekwa kujifunza katika mfumo mwingine utakaomwwezesha ajifunze kusoma na kuandika.
Alisema mwaka huu wizara ilijipanga kabla ya kufanyika kwa mtihani ambapo kila shule ilikaguliwa kama wanafunzi wanaofanya mtihani wana sifa zinazostahili.
Aliongeza kuwa mkakati mwingine uliowekwa na wizara ni kuwezesha wanafunzi kufanya mtihani wa aina moja kwa lengo la kuchuja wasiojua kusoma na kuandika.
“Tulibaini tangu mwanzo kungekuwa na njama za baadhi ya wazazi kutumia mbinu chafu kuwezesha watoto wao wafaulu, lakini tulijipanga kukabiliana na tatizo hilo kwa hiyo siyo rahisi mwaka huu ikajitokeza mwanafunzi aliyechaguliwa akawa hajui kusoma wala kuandika,” alisema Dk. Kawambwa.
MFUMO MPYA WALETA UFANISI
Waziri Kawambwa akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu mfumo mpya wa usahihishaji unajulikana kama ‘Optical Mark Reader’ (OMR) ulivyotumika kwa mara ya kwanza, alisema umekuwa na mafanikio makubwa.
Alisema mwaka 2011 wizara ilitumia walimu 4,000 kwa ajili ya kusahihisha mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa muda wa mwezi mmoja, lakini mwaka huu kwa kutumia mfumo huo kwa mara ya kwanza, ni walimu 285 tu waliotumika kusahihisha mtihani huo kwa muda wa siku 15.
”Walimu ndio wanatunga mtihani wa darasa la saba kwa hiyo sidhani kama wanaweza tena wao wenyewe wakaanza kulalamikia mfumo wa OMR ambao umeonyesha mafanikio makubwa na unatumika katika nchi nyingi duniani,” alisema Dk. Kawambwa.
Kwa mujibu wa mfumo huo wa usahihishaji, watahiniwa walitumia fomu maalum za teknolojia kujibia maswali ambazo zilitumika kusahihishwa kwa mashine maalumu.
Mfumo huo una lengo la kupunguza ubabaishaji wa matokeo kwa ujumla kwa watahiniwa.
Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) awali lilisema kuwa mfumo huo ni mzuri na waliufanyia majaribio na unatumika katika nchi nyingi kwa lengo la kupunguza uchakachuaji na gharama za kusahihisha mitihani hiyo.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi, Waziri Kawambwa alisema wizara yake itafanya uchunguzi kubaini kama kuna ukweli kwamba wapo wanafunzi wenye ulemavu ambao wameshindwa kurejea kwao kwa kukosa nauli.
HALMASHAURI ZAAGIZWA
Katika hatua nyingine, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeziagiza Halmashauri kote nchini kwa kushirikiana na wadau wengine kukamilisha ujenzi wa majengo na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2013.
Dk. Kawambwa alisema wazazi, walezi na jamii washirikiane na uongozi wa wilaya, halmashauri na shule kuhakikisha wanafunzi waliochaguliwa wanaandikishwa, wanahudhuria na kubaki shuleni hadi watakapohitimu elimu ya sekondari.
Aidha, Waziri Kawambwa aliwataka wanafunzi waliochaguliwa kutumia fursa hiyo vizuri katika kujifunza.
Vile vile, aliwataka walimu na watendaji wa elimu kuongeza bidii katika usimamiaji na ufuatiliaji wa utoaji wa elimu ili kuboresha elimu nchini.
No comments:
Post a Comment