Mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima,
Shaban Matutu, akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhmbili
jijini Dar es Salaam jana baada ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na
polisi.
Matutu (30), ambaye amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) Muhimbili, alikumbwa na mkasa huo baada ya askari wanne waliovalia kiraia kuvamia nyumbani kwake, Kunduchi Machimbo, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, saa 3.30 usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha mwandishi huyo kujeruhiwa kwa risasi.
KAULI YA MWANDISHI
Akizungumza na NIPASHE akiwa Moi jana, Matutu alisema baada ya askari hao kuvamia nyumbani kwake waliita jina la mkewe anayefahamika kwa jina la mama Jumanne.
“Walimuita mke wangu akaitikia, wao wakamtaka atoke nje, mimi nikawajibu nakuja. Nilitoka nikiwa nimeshikilia panga kwa tahadhari, nilipofungua mlango niliona watu wengi nikamtahadharisha mke wangu kuwa huku si salama,” alisema Matutu na kuongeza:
“Nilimuamuru arudi nyuma, mimi nikaufunga mlango haraka, lakini wao (polisi) waliung’ang’ania na kunipiga risasi kwenye kiganja cha mkono wa kushoto na kupitiliza hadi begani, huku wakitulazimisha tukae chini.”
Kwa mujibu wa Matutu, wakati anapigwa risasi, hakujua kama amejeruhiwa.
Badala yake, alisema aliposikia mlio wa risasi, alimuuliza mkewe kama yuko salama, lakini baadaye aligundua kuwa damu nyingi ilikuwa inachuruzika.
Alisema polisi hao walidai walifika nyumbani kwake kumtafuta Mama Jumanne, anayeuza pombe haramu aina ya gongo, lakini bahati mbaya walifika eneo, ambalo silo.
“Walinichukua hadi kituo cha polisi wakaniandikia fomu namba tatu (PF3) wakanipeleka Hospitali ya Mwananyamala, ambako ilishindikana, wakanileta hapa MOI,” alisema Matutu, ambaye hadi jana asubuhi alikuwa bado hajapatiwa matibabu.
Hata hivyo, baadhi ya madaktari walishangazwa na kitendo cha askari hao kuondoka na maelezo ya mgonjwa ikiwa ni pamoja na PF3, kitendo walichodai ni kupoteza ushahidi.
Matutu alisema polisi hao walikuwa wakihaha kutafuta suluhu ya tukio lao la kizembe walilomfanyia, huku wakimsisitiza kuwa akitoka hospitalini wawasiliane ili waone ni namna gani wanaweza kumalizana.
Afisa Uhusiano wa Moi, Jumaa Almasi, alithibitisha kumpokea mgonjwa huyo juzi usiku majira ya saa nane akiwa amepigwa risasi.
Alisema alifanyiwa upasuaji na kuondolewa risasi iliyokuwa mwilini na amelazwa katika wodi ya Sewahaji namba 17 na kwamba, anaendelea na matibabu.
MAELEZO YA POLISI
Wakati Matutu akitaja sababu ya askari hao kuvamia nyumbani kwake kuwa ilikuwa ni kumtafuta mama Jumanne anayefanya biashara ya kuuza gongo, Kamanda Kenyela aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa askari hao walivamia nyumba hiyo kuwasaka ili kuwakamata majambazi.
Kamanda Kenyela alisema katika tukio hilo, askari mwenye namba F. 8991 D/C Idrisa alijeruhiwa kwa kukatwa na panga kwenye mkono wake wa kulia.
Alisema baada ya kujeruhiwa, askari huyo aliyekuwa na bastola alirukiwa na Matutu.
Kamanda Kenyela alisema katika tafrani hiyo, risasi ilifyatuka kutoka kwenye bastola hiyo na kumjeruhi Matutu kwenye bega la kushoto.
“Baada ya kitendo hicho kutokea ndipo ilifahamika kuwa mtu aliyekuwa anapambana na askari jina lake ni Shaban Matutu, mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima, mkazi wa Kunduchi Machimbo,” alisema Kamanda Kenyela.
Alisema baada ya tukio hilo, askari na mwandishi huyo walikimbizwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.
Kamanda huyo alisema baadaye Matutu alipelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi na kwamba, hali za wote wawili zinaendelea vizuri.
Alisema katika tukio hilo, askari hao walifika kwenye nyumba hiyo kufuatia taarifa kutoka kwa msiri kuwa katika nyumba ya mama ‘J’ iliyoko Kunduchi Machimbo kuna majambazi hatari.
“Ndipo katika ufuatiliaji huo katika nyumba hiyo akajitokeza Shaban Matutu na kumjeruhi askari kwa panga na hatimaye yeye pia akajeruhiwa kwa risasi,” alisema Kamanda Kenyela.
Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini sababu za askari kushambuliwa na kujeruhiwa.
Hata hivyo, Kamanda Kenyela katika hali ya kushangaza hakusema kama kuna uchunguzi wowote unaofanywa kubaini sababu za mwandishi huyo kujeruhiwa kwa risasi na askari huyo.
Badala yake, aliwaomba wananchi kutii sheria za nchi ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza pindi watu wanapochukua sheria mikononi.
Pia aliwaomba wananchi kuliamini Jeshi la Polisi na hivyo watoe ushirikiano katika kupambana na uhalifu licha ya changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Pale ambapo mtu au kikundi cha watu kitakapoona kuwapo kwa uonevu au taratibu zisizo za kisheria miongoni mwa askari wanapokuwa kazini ni vyema wakatoa taarifa kwa viongozi husika ili hatua stahili zichukuliwe badala ya wananchi kujichukulia sheria mikononi,” alisema Kamanda Kenyela.
TEF WALAANI
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, alieleza kusikitishwa kwake ni vitendo vya uvunjaji wa haki dhidi ya wanahabari nchini ambavyo vimeendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na kutaka polisi waliofanya hivyo kuchukuliwa hatua kali.
Kibanda alisema wakati Taifa likiwa bado katika majonzi ya mauaji ya kinyama ya aliyekuwa Mwandishi wa Channel Ten mkoa wa Iringa, Daudi Mwangosi, unashuhudiwa tena unyama mwingine dhidi ya mwanahabari.
Alisema ikiwa Jeshi la Polisi litakosa majibu kuhusiana na sababu za kumpiga risasi mwanahabari huyo, utafika wakati wanahabari nchini watalichukulia Jeshi la Polisi ni hatari kwao.
FREE MEDIA YANENA
Naibu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media, inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Ansbert Ngurumo, alisema kuwa wanaiomba mamlaka husika kufuatilia juu ya utendaji kazi wa Polisi wanaowapeleka katika kutekeleza shughuli mbalimbali.
“Kwa kweli inasikitisha kwani matukio haya sasa yanaonekana kufululiza, polisi wanavuka mipaka, si muda mrefu tangu kuripotiwa kwa kifo cha mwandishi wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, leo kijana wetu na hatujui kesho atakuwa nani, inasikitisha kwa kweli,” alisema Ngurumo.
No comments:
Post a Comment