Saturday, October 20, 2012

Waandamanaji 53 mbaroni,baadhi wapenya na kutinga Ikulu

****JWTZ yadhibiti mitaa Kariakoo, maduka barabara zafungwa

picha zikiwaonyesha waandamanaji waliodhibitiwa.....

Magari ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) yakiwa yamepakia wanajeshi tayari kukabiliana na waandamanaji wa Kiislamu eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam jana.
Jiji la Dar es Salaam jana lililipuka hata kulazimika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuingilia kati na kuongeza nguvu kudhibiti  vurugu kubwa zilizotikisa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, zilitokana na maandamano ya baadhi ya waumini wa Kiislamu waliokuwa wanataka kwenda Ikulu.
Magari kadhaa ya JWTZ yaliyosheheni askari  wa jeshi hilo yaliranda katika mitaa mbalimbali ya  jiji  na eneo la Wizara ya  Mambo ya Ndani  na  Ikulu  huku helkopta ya polisi ikiwa angani kufuatilia usalama wa eneo hilo.
Askari wa JWTZ waliingilia kati kusaidia jeshi la polisi lililoonekana kuzidiwa nguvu baada ya waandamanaji hao kupambana na polisi hao kwa kuwarushia mawe.
Askari hao waliokuwa na silaha, ikiwemo mabomu ya machozi, maji ya kuwasha na risasi za moto, walitanda katika maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.
Maandamano na vurugu hizo zilisababisha shughuli mbalimbali  hasa biashara na usafiri kusimama huku wafanyakazi wa maeneo ya mjini kuondoka mapema maofisini.
Waumini hao waliandamana  kuishinikiza  serikali imuachie huru  Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislam Tanzania  Sheikh Issa  Ponda, aliyefunguliwa mashtaka ya uchochezi pamoja na waumini wengine kadhaa walioko mahabusu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, pamoja na Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadik, kwa nyakati tofauti waliwasihi waumini kutawanyika mara baada ya kumaliza ibada ya Ijumaa jambo ambalo baadhi ya Waislam hawakuliafiki.
Askari wa JWTZ  hawakujihusisha na kamata kamata  ama kupambana na waandamanaji moja kwa moja lakini walikuwa nyuma ya polisi kuhakikisha kuwa pale nguvu inapopungua wanaingilia .
Pamoja na askari wa  JWTZ, Vikosi  vya  Kutuliza Ghasia  (FFU),  vikishirikiana na  askari wa vikosi vya  mbwa pamoja na wanamgambo wa jiji walikabiliana na maandamano yaliyoanza baada ya swala ya Ijumaa.
KUPAMBANA NA WAANDAMANAJI
Katika vurumai hizo polisi walitumia virungu, mabomu ya machozi, maji ya kuwasha huku wengine wakiwa na bunduki na risasi za moto kuwatawanya waandamanaji ambao walijibu kwa kuwarushia mawe na vitu vingine.
Licha ya kuwa na vurumai hizo  gari la polisi lilitoa tangazo kwa wanausalama kufanya kazi yao kwa tahadhari na kukataza ukamataji watuhumiwa na kudhibiti vurumai usitumie risasi za moto  na mabomu ya machozi yaliyokuwa yanarushwa yasielekezwa kwa raia.
Kadhalika polisi  waliuzingira  msikiti wa Idrisa ulioko karibu na kituo cha Polisi cha Msimbazi  kufuatia idadi kubwa ya waandamanaji kukimbilia humo. Ili kuwatoa waliokuwa  mafichoni  polisi walimwaga maji ya kuwasha ili kuwatoa waandamanaji walioingia ndani kwa  kuruka ukuta.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji  waliokuwa wametanda barabarani hali iliyosababisha barabara  kadhaa zikiwemo za Kariakoo, Kinondoni, Kawawa na Morogoro kufungwa.
Mathalani watu walishindwa kupita kwenye barabara ya Kinondoni inayoungana na ile ya Kawawa kutokana na polisi kudhibiti maandamano hayo na kusababisha njia hiyo isipitike.
KARIAKOO YALIPUKA
Kariakoo,  ambayo kiuchumi ni  kitovu kikubwa cha biashara za Tanzania jana ilizizima  kwa moshi na kelele za mabomu na kusababisha  biashara za mabenki, maduka ya fedha, soko kuu la vyakula  na bidhaa za walaji kufungwa kwa muda wote.
Pia ofisi na vioski zinapouzwa bidhaa na huduma mbalimbali vilifungwa  kwenye  sehemu nyingine za mitaa  ya katikati ya jiji zilizohofiwa kukumbwa na  vurumai hizo.
Eneo hili halikuwa shwari kwani wananchi wakiwemo wanafunzi walijikuta katika wakati mgumu huku wangine wakipigwa na mgambo wa jiji  na kuishia mikononi mwa polisi wa FFU.
Uharibifu wa mali ulitikisa kwa kuchoma matairi katikati ya  barabara pamoja na wezi kupora kwa urahisi bidhaa zilizokuwa maeneo ya wazi.
NIPASHE iliyokuwa eneo la tukio, ilishuhudia malori ya polisi yenye namba PT 18448 , PT 2093, PT 1145 na T662 APM yakiwa yamebeba watuhumiwa na gari la  makachero wa upelelezi yakisomba watu kadhaa waliokamatwa kwenye vurumai hizo na kuwapeleka  kituo cha Msimbazi .
Walioshikiliwa watabakia rumande hadi Novemba Mosi wakisubiri maamuzi ya hatua zitakazochukuliwa. Kadhalika polisi walifanya msako wa nyumba kwa nyumba ili kuwakamata waliokuwa  wanapambana nao wakiwa majumbani.
TISHIO LA MAISHA
Wakati huo huo  vurugu hizo zimesababisha mwanamke  mmoja ambaye hakufahamika kuzirai na kupoteza fahamu kufuatia milipuko ya mabomu ya kutoa machozi iliyorindima Kariakoo.
WANANCHI WALAANI
Watu mbalimbali  wamelaani tukio hilo na kuitaka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanaosababisha vurumai  kwani zinahatarisha amani ya nchi
Kwa upande wake, Skeikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Sheikh Alhadi Salum aliwaomba Waislamu kuacha kuandamana na kwamba waliache sheria ichukue mkondo wake  na suala la dhamana   ni haki ya kila mmoja, hivyo watapatiwa.
Viongozi wa dini walitoa wito wa kutafuta suluhu kwa kuaa pamoja ili kufikiana muafaka.
KOVA ALONGA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova, akizungumzia vurumai za jana  alisema hakuna polisi wala raia aliyepoteza maisha jana.
Kova aliongeza kuwa waliokamatwa ni  kutokana na vurugu hizo ni 53 na kwamba walitiwa mbaroni baada ya kukaidi amri ya serikali ya kuwataka wasiandamane . Katika hatua nyingine alisema waliojeruhiwa ni wale waliokimbia ovyo.
Alisema hakuna risasi zilizotumika mbali na mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kudhibiti vurugu hizo.
NCHIMBI ATETA NA VIONGOZI WA ULINZI
Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emmanuel Nchimbi, jana alikutana na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wa wizara  hiyo. Habari  tulizozipata kabla ya kwenda mitamboni zilisema.
JK ATOA POLE
Rais  Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema kuomboleza kifo cha askari polisi  Said Abdulrahman  aliyuawa  kikatili visiwani  Zanzibar.
Abdulrahman wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), aliuawa kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi usiku wa Jumatano wiki hii  katika eneo la Bububu  wakati akirejea nyumbani baada ya kazi kazi.
 “Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kuuawa kikatili kwa askari wetu Said Abdulrahman wa kikosi cha Kutuliza  Ghasia usiku wa tarehe 17 Oktoba wakati  akirejea nyumbani kwake, baada ya kukamilisha zamu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao kwa siku hiyo,” alisema Rais Kikwete.
“Kitendo hiki cha mauaji ni kitendo kiovu, ni cha kikatili na kinachostahili kulaaniwa na kufanyiwa kila aina ya uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria haraka iwezekanavyo,” alisema Rais Kikwete katika salamu hizo.
Alisema anaungana  na familia hiyo kumwomba Mwenyezi Mungu, ailaze roho yake mahala pema peponi .

HOSPITALI YA AMANA
Majeruhi tisa wa vurumai hizo walifikishwa katika hospitali ya Amana ambapo nane kati yao walitibiwa na kuruhusiwa wakati mmoja Neema Samson (26) amelazwa.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment